March 20, 2017



Na Saleh Ally
TAARIFA ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia kituo cha runinga na Clouds usiku wa juzi, kimekuwa gumzo zaidi.

Watu wengi wamekuwa wakikijadili mitandaoni kupinga kuhusiana na suala hilo ambalo hakika kweli ni la kulaaniwa.

Uongozi wa Clouds Media Group kupitia Mkurugenzi wake wa Vipindi, Ruge Mutahaba na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu, Joseph Kusaga, tayari wamelaani.

Wakati Clouds wakilaani kuhusiana na hilo, kwanza nianza kuungana na wao kwa kuwapa pole kuwa ni moja ya jambo baya kabisa limewatokea.

Jambo hilo, linaonyesha kiasi gani viongozi wa serikali, wanaweza kupotosha au kupotoka katika suala la maadili.

Kwa mujibu wa Clouds ambao wamekuwa kipenzi cha marafiki wa Makonda, wamesema alivamia akihoji ni kwa nini hasa ishu ya mwanamke aliyekuwa akidai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Makonda alipenda kuona kipindi cha De Weekend Chat Show’ maarufu kama Shilawadu kinaonyesha jambo hilo. Ajabu zaidi akachota sehemu ya kipindi ambayo haikuonyeshwa na kuondoka nayo.

Hauwezi kuamini kama mkuu wa mkoa fulani au kiongozi mwenye dhamana ya wananchi anaweza kufanya jambo la hovyo kama hilo.

Lakini ninashangazwa kuona Wanahabari wakiwa kimya bila ya kukemea. Kuna njia sahihi ya kupita na kukemea bila ya woga hata kidogo.

Waandishi hawapaswi kuwa waoga, wala hawapaswi kuhofia kuwekwa ndani au kunyanyazwa kwa kuwa watamkoa Makonda.

Waandishi wa habari nao ni wananchi, wana haki zao na wana haki kama waandishi. Makonda anapaswa kuiheshimu hii tasnia hata kama ana dhamana ya cheo ambacho ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Si sahihi kiongozi kuanza kukipangia chombo cha habari kurusha kitu kwa ajili ya faida yake yeye, tena katika vita ambayo anataka kujifaidisha yeye hata kama hakuna weledi.


Makonda anapaswa kuelezwa amakosea, anapaswa kuelezwa hakuwa sahihi hata kidogo na asithubutu kurudia madudu aliyoyafanya.

Jiulize, kama wanahabari nao mtakuwa waoga kusema, kesho nani atazungumza wananchi wanatapoonewa.

Hofu ya ukionyesha unampinga Makonda unaweza kutengenezewa janga, mfano unauza unga au umefanya jambo baya iondoeni kabisa na nisisitize. Tasnia ya habari iheshimiwe si na Makonda tu ambaye tayari ameonyesha dhahara sana, bali viongozi wengi wa serikali.


Nimpongeze Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye ameunda kamati ya saa 24 ambayo itachunguza suala hilo.

Lakini niwapongeze Moat ambao Mwenyekiti wao, Reginald Mengi amejitokeza na kukemea. Ameungana na Clouds katika wakati huu wa hovyo kabisa kuwahi kutokea katika nchi yetu kwa kiongozi wa mkoa kuona yuko juu ya kila kitu.

Niwapongeze Waziri Nape na mzee Mengi kwa kuonyesha wanajali. Niwasisitize waandishi wasiwatengeze Clouds hata kama walikuwa na tofauti nao.

Tumeona, Majizo ambaye ni mmiliki wa EFM, amewapigia Clouds na kuwa pole. Mimi nilifika Clouds na kuwapa pole pia.


Lakini mwisho niwakumbushe, vizuri pia kuungana inapofikia wakati wa kukosoa. Kila alipokosea Makonda, Clouds walimsafisha. Leo amewaonyesha upande wa pili wa shilingi kwamba hakupaswa kutetewa hata kidogo. Hivyo hili liwe somo kwao, kwetu na kwa wengine. Kwamba wanaokosoa kwa nia nzuri hasa kunapokuwa na uozo, nao waungwe mkono.

Huu ni wakati wa kuungana na kupinga hili. Simshauri hata mmoja kwenda nje ya sheria za nchi, lakini kwa mujibu wa sheria waandishi tuna njia sahihi ya kupita na kukemea bila ya woga, bila kutishwa wala kubabaisha.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic