March 20, 2017




Na Saleh Ally
WAKATI Watanzania wengi sasa wamekuwa wakitamani siku moja kuwaona wachezaji kutoka nchini wakicheza katika Ligi Kuu ya England, wachache wanajua ugumu unaotokana na kiwango cha soka nchini unavyoweza kuzuia ndoto zao hizo.

Mtanzania ambaye anaonekana ana nafasi kubwa ya kucheza soka nchini England ni Mbwana Samatta ambaye anakipiga katika Klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji.
Samatta anacheza Ubelgiji ambako kiwango cha soka kwa mujibu wa viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kipo juu sana. Ubelgiji inashika namba tano katika viwango hivyo vya Fifa.

Lakini Samatta anatokea katika nchi ambayo kiwango chake ni namba 157 ambalo ni jambo gumu sana kwake kuvuka hadi England hadi atakapofikia masharti magumu ambayo yamewekwa na Chama cha Soka England maarufu kama FA.


Kuna mengi yanatakiwa kufanyika hadi mchezaji anayecheza Tanzania au Afrika Mashariki aweze kufikia ndoto yake ya kucheza England. Anaweza kupata msaada mkubwa kama atapitia njia za mkato kukwepa sheria kali za FA kwa wachezaji wanaotokea nje ya Bara la Ulaya na hasa katika Jumuiya ya Ulaya.

Kucheza katika nchi zilizo ndani ya umoja huo, kunasaidia mchezaji kuonekana ana nafasi ya kusogea ingawa bado kumekuwa na ugumu kama wataangalia kiwango cha nchi yake kipo chini sana kwa kuwa FA wamepitisha mchezaji mwenye nafasi ya moja kwa moja kutoka nje ya eneo lao au Umoja wa Ulaya (EU), basi lazima nchi yake iwe kuanzia namba moja hadi 50 katika viwango vya Fifa.



Kitengo cha wanaotokea nje ya umoja huo au “Non-EEA (European Economic Area)/ EU (European Union) football players” wanaonekana ni kama wale wanaokwenda kuziba nafasi ya vipaji vya walio ndani ya jumuiya hiyo, ndiyo maana masharti yamekuwa makali.

Kwa kifupi, Waingereza wanajua faida ya kucheza Premier League. Kwanza wanaangalia timu yao ya taifa, faida ya kipato pia. Ndiyo maana wanahakikisha kuna ugumu wa juu kwa wachezaji kutoka Afrika, Asia, Urusi, Amerika Kusini na kadhalika.


Lakini Amerika Kusini wanakuwa na nafasi kubwa kwa kuwa kwa Fifa wengi viwango ni juu. Lakini bado, wanajitahidi kuwabana na masharti kama yafuatayo.



Sheria ya 1:
Mchezaji angalau anatakiwa kuwa amecheza mechi kwa asilimia 75 katika timu yake ya taifa, hii iwe katika kipindi cha ndani ya miaka miwili.
Lakini nafuu iko hivi; kama nchi iko katika kiwango kutoka 1-10, basi uwe umecheza angalau 30% za mechi za timu ya taifa, 11-20 awe amecheza hadi 45%, 21-30 hadi 60% na 31-50 hadi 75%.

Katika nchi za Afrika Mashariki hakuna hata nchi moja ipo katika kiwango hicho na Uganda ambao ndiyo best, wao wako katika 74. Ndiyo maana utaona David Obua alikwama kujiunga na West Ham United wakati akitokea Hearts ya Scotland, licha ya kwamba nchi hiyo iko ndani ya Uingereza.

Juhudi za kukata rufaa za West Ham, ziligonga mwamba.
Victor Wanyama naye alipata wakati mgumu wakati anatokea Celtcs kujiunga na Southampton kwa kuwa Kenya ilikuwa katika nafasi ya 106 wakati huo katika viwango vya Fifa.

Kilichomsaidia ni kwamba alicheza mechi za timu ya taifa katika mechi za mashindano na zile za kimataifa chini ya Fifa na Caf kwa 100%. Hii ilichangia kuwazima FA ambao mwisho walikubali.



Sheria namba 2:                                                                                  
 Sheria nyingine ni kwamba kwa wale ambao wamo ndani ya 70 ya viwango vya ubora vya Fifa, wao wanatakiwa kuwa katika kikosi cha timu ya taifa kwa angalau miaka miwili mfululizo bila kukosa kila kinapotangazwa.


Hii ilikuwa kama mlainisho wa sheria ya kwanza, kwamba wachezaji ambao nchi zao hazimo ndani ya 50 Bora ya Fifa, basi wanaweza kukatazwa kwa ujumlisho. Kwamba wanacheza kwenye ligi ambayo kiwango cha nchi hiyo kipo juu, lakini wao wanashiriki michuano ya kimataifa kwa upana zaidi. Hii kidogo inaweza kuwa na mlegezo kwa Tanzania na nchi nyingine kama Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.

FAIDA KWA SAMATTA:
Samatta ni kati ya wachezaji wenye nafasi kubwa ya kwenda kucheza England kama kiwango chake KRC Genk kitaendelea kuimarika na kuendelea kufanya vema. 

Anacheza katika nchi ambayo kiwango chake ni namba tano lakini utaona kwamba anafanya vizuri zaidi katika kikosi cha timu ya taifa na ushiriki wake ni asilimia 100%.
Ndiyo maana unaweza kushangaa, Samatta anasafiri hadi Dar es Salaam kujiunga na Taifa Stars hata kama ni mechi za kirafiki ambazo unaziona za kawaida. Yeye anakuwa anajua nini kinatakiwa na afanye nini itakapofikia wakati wa kuvuka kwenda mbele.


Lakini utagundua kuna ugumu wa juu kabisa kwa wachezaji wengi ambao wapo katika nchi ambazo si za Ulaya na hasa Umoja wa Ulaya (EU). Kwamba kwenda England si safari rahisi, hata kama ligi ni ngumu, wahusika wamejenga uzio mkuu kuhakikisha wanalinda wachezaji kutoka nje kwenda England.


Wanataka kutoa nafasi kwa vijana wao kukua na kufaidika na matunda ya ligi yao ambayo inaingiza mabilioni ya fedha. Hivyo kwa mchezaji Mtanzania, hawezi kutoka moja kwa moja kwenda kujiunga na Man United, Arsenal au Liverpool. Lazima kuwe na mzunguko na kuanzia nchi nyingine za Ulaya ndiyo jibu.

UMUHIMU:
Lakini kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao wanataka maendeleo basi wao pia wanapaswa kujua kwamba wanahusika na ukuaji wa soka la nyumbani na umuhimu wa viwango vya Fifa.

Kama vinapanda ni kufungua njia kwa wachezaji wetu na si kusisitiza wanatakiwa kwenda nje huku mdororo unaosababishwa na viongozi unazidi kupaa na kupanda kwa kuwa viongozi ni dhaifu, wanalinda matumbo yao na wana uhakika wa kuendelea kuongoza kwa kuwa wanajua wapiga “kura” ni mali yao. Hii si sawa hata kidogo.

TIMU YA TAIFA:
Kwa wale wanaocheza timu ya taifa, wasifikiri Taifa Stars ni klabu au ni sehemu ya kwenda kujiburudisha tu. Wajue kuiinua ndiyo itakayowabeba baadaye. Kuifanya Taifa Stars ifanye vizuri, maana yake Tanzania itafanya vizuri na kujitangaza na baadaye itasaidia kufungua milango kwao.


Unapopata nafasi ya kuichezea Taifa Stars, fikiria mambo mengi sana ya mbele, acha ubishoo na kuona ni mambo ya kawaida tu. Pia makocha, wajue hili ni jukumu lao na kama kuna wachezaji ambao wanaona wanaleta mzaha, tupa kule na wasirudi kabisa kwa kuwa mechi moja ya Taifa Stars, maana yake ni kubwa kuliko dakika 90 pekee za mchezo. Kuzidiwa hadi na Rwanda katika viwango, Kenya na Uganda wanazidi zaidi ya nafasi 40, huu ni uzembe wa hali ya juu unaostahili adhabu kali!

 VIWANGO VYA UBORA FIFA:
England 14

AFRIKA NDANI YA 50 BORA:
Misri 20
Senegal 28
Cameroon 32
DRC 38
Nigeria 41
Ghana 43
Ivory Coast 47
Algeria 50


AFRIKA MASHARIKI:
Uganda 74
Kenya 88
Rwanda 93
Tanzania 157
*Wanachama wote 205

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic