March 28, 2017



Na Saleh Ally
KIPAJI ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini inawezekana kuna watu wengi wana vipaji na hawajawahi kuvigundua ni vya kitu gani.

Kitaalamu inaonyesha hivi, mara nyingi kipaji cha mwanadamu hujulikana kulingana na anavyopewa nafasi ya wazi kufanya jambo fulani.

Anayefanya jambo kwa uhuru akiwa na umri mdogo anakuwa na nafasi ya kuonyesha uwezo wake au kipaji alichonacho na kuanzia hapo, ndipo walio karibu yake wanakuwa na nafasi ya kukiendeleza.



Asilimia 72 ya wanaofanya vizuri kupitia vipaji walipewa nafasi wakiwa wadogo. Asilimia 16 tu ndiyo vipaji vyao viligunduliwa na watu wengine kutokana na umakini wao lakini asilimia 81, wamegunduliwa vipaji vyao wakiwa wamechelewa kabisa na asilimia 12, walichelewa lakini bado vipaji vyao vikaweza kutumika.

Inawezekana kabisa, watoto wengi wa Kitanzania vipaji vyao vimepotea kutokana na malezi ya aina moja ya Watanzania wengi na wazazi kuendelea kuiga yaleyale waliyoyaona kwa wazazi wao bila ya kuwa na ubunifu wao binafsi ili kuboresha maisha kulingana na wakati husika.

Oratilwe Hlongwane ametimiza miaka minne na ushee na sasa yeye ndiye binadamu tajiri zaidi kuliko yeyote katika familia yao.

 Anaingiza mamilioni ya fedha kupitia katika makampuni mbalimbali yakiwemo makubwa ya utengenezaji wa magari kutokana na ubora wa kazi yake.



Hlongwane ni mchezesha muziki, maarufu zaidi kama Disco Joker au DJ na anajulikana dunia nzima sasa kwa jina la utani la DJ Arch Jr.

DJ Arch Jr aliyeanza kujulikana kwa jina la DJ AJ, ameingia mkataba na Kampuni ya Kimarekani ya kutengeneza “Headphones” na “Earphones” ya Beats. Mmiliki wake ni mwanamuziki nguli wa hip hop na milionea, Dr Dre.

Si kazi rahisi kuingia mkataba na kampuni hiyo lakini hii inatokana na namna DJ Arch Jr alivyoweza kuonyesha kipaji chake cha kuchezesha muziki, akianzia kupata umaarufu katika Tamasha la South Africa Got Talent ambalo aliibuka mshindi akiwa na umri wa miaka mitatu tu na kubeba kitita cha Rand 500,000 (Sh milioni 87.3).



Pia DJ Arch Jr ana mkataba na Kampuni ya Djay Software ambayo hutumika kujifunzia masuala ya Udj. Kampuni nyingine ni Guess Kids pamoja na Mini Cooper ambao wanatengeneza magari ya aina hiyo.

Hii inamfanya kuwa mtoto tajiri zaidi nchini Afrika Kusini kwa kuwa kwa mwaka anaingiza hadi Rand milioni 19 (Sh bilioni 3.3) kupitia mikataba yake na ana uwezo wa kuingiza hadi Rand milioni 25 (Sh bilioni 4.3) kama atajumlisha fedha anazolipwa kwenye shoo zake.

DJ Arch Jr anatokea katika familia ya kawaida kabisa. Baba yake mzazi Glen Hlongwane ambaye ni mwalimu wa sarakasi aliamua kununua kompyuta mpakato au ipad kwa ajili ya kukuza uelewa kwa mwanaye mdogo akiwa na mwaka mmoja tu.

Aliona kwa kuwa anapenda muziki, basi ni vizuri kuweka ‘application’ ya kufundisha Udj ya DJ App. Taratibu akawa anaitumia na baadaye akaonekana kuipenda sana. Mara nyingi alikuwa busy akichezesha kichwa na kumfanya asiwe na marafiki zaidi ya kuitumia.



Mama yake mzazi, Refiloe Marumo anasema mwanaye DJ Arch Jr alikuwa akiwashangaza awali na alikwenda akizidi kujifunza hadi baba yake alipompa ruhusa kutumia mashine ya Udj aliyokuwa akifanyia mazoezi kama sehemu ya kujifurahisha.

Baba yake alinunua mashine hiyo kwa kudunduliza sana fedha zake ili apate muda wa kuwa nyumbani na familia yake wakati akiichezea.

Alianza kushangazwa na DJ Arch Jr alipokuwa akifanya vizuri na kutumia muda mwingi zaidi akiichezea. Ajabu zaidi akawa anajua kuchagua aina ya mpya za muziki au unaotamba kipindi husika.

Wazazi wake baadaye walianza kupata lawama kwa majirani na watu wa eneo walilokuwa wakiishi kwamba wanamfanya mtoto wao kama mtaji.

Wao walisema hawamlazimishi, akikua ana uwezo wa kuchagua kazi anayotaka, wataendelea kumpa nafasi ya kufanya anachotaka na kumuunga mkono juu.

Wanadamu hawaishi lawama, kila utakachofanya bila kujali kizuri au kibaya, watalaumu.

Kipaji cha DJ Arch Jr, sasa kinaiendesha familia yake ambayo imehamia katika eneo lenye makazi bora jijini Johannesburg ukilinganisha na walivyokuwa wakiishi awali na hii yote kwa kuwa walitoa nafasi kwa mtoto wao kipaji chake kuonekana. Kama wewe ni Mzazi Mtanzania, lifikirie hili.

Sasa wasanii wakubwa wa Marekani wenye fedha nyingi, wanatamani kufanya naye kazi katika siku za usoni.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic