May 20, 2017Kipa mkongwe wa zamani Yanga, Simba na Taifa Stars, Ivo Mapunda amesema kitu kinachowafanya wachezaji wengi wa Tanzania wasifanikiwe katika maisha ni kupoteza muda mwingi na timu.

Akizungumza katika kipindi gumzo cha michezo cha Spoti Hausi kinachorushwa moja kwa moja na Global TV Online, Ivo alisema kitendo cha wachezaji kutumia muda mwingi kambini kinawanyima nafasi ya kufanya vitu vingine vya maendeleo yao.

“Sisi wachezaji wa Tanzania tunashindwa kufanikiwa kwenye maisha yetu nje ya soka kwa sababu hatuna muda wa kufanya hata biashara, muda mwingi tunautumia kambini au mazoezini.

“Biashara inahitaji usimamizi wa kina kidogo, sasa unaweza kufungua biashara na ukala hasara kwani unakosa muda wa kuisimamia vizuri na kama umemkabidhi mtu asiye mwaminifu ni tabu,” alisema Ivo.

“Ndiyo maana utakuta wachezaji wengi walipata fedha lakini wameshindwa kujiendeleza kwa kuweka vitega uchumi.”

Ivo alisema wakati anachezea Gor Mahia ya Kenya hawakuwa na utaratibu wa kambi kwa muda mwingi na hata siku za mechi walikuwa wakitokea majumbani mwao.

“Gor Mahia kambi si ya muda mrefu, hata siku ya mechi mara nyingi tulitokea nyumbani, tulikuwa tunapata muda mwingi wa kufanya mambo yetu mengine ya maendeleo tofauti na hapa Tanzania,” alisema Ivo ambaye sasa anamiliki kituo cha kukuza vipaji cha Ivo Mapunda Sports Centre.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV