May 1, 2017




Na Saleh Ally
KIKOSI cha Mbao FC kimeandika rekodi ya kuwa timu iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu wa kwanza na inakwenda kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho.

Wakati ndiyo wamepanda, wameonekana kama kiboko cha vigogo na mwisho wamefanikiwa kuweka rekodi ya kuwavua ubingwa wa Kombe la Shirikisho, Yanga.

Wamewafunga Yanga kwa bao 1-0 katika mechi ya pili ya nusu fainali kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, jana.

Wakati Mbao FC wanaivua ubingwa Yanga huku wakionyesha soka bora kabisa, moja kwa moja inaonyesha mengi sana ambayo kama wadau wa soka tunaweza kujifikiria na kupambanua.

Mbao FC ilipanda ligi kuu kwa rundo la mizengwe baada ya baadhi ya timu zilizotuhumiwa kupanga matokeo kupatikana na hatia na kupokwa pointi.

Bila adhabu na kuibuka kwa ishu hizo, Mbao FC isingepata nafasi ya kupanda na huenda isingekuwa na morali ya kupambana na timu kama Yanga jana. Morali imepatikana kutokana na uzoefu wao katika Ligi Kuu Bara ambao wameupata baada ya kucheza na timu kadhaa bora.

Lakini nataka pia nikukumbushe kwamba uchezaji wa wachezaji wa Mbao FC umeonyesha ni kikosi kinachoundwa na wachezaji wasio na majina lakini wenye malengo ya kutaka kushinda.

Wanaoendesha klabu ya Mbao ni wauza mbao wa Jiji la Mwanza ambao walijitolea kuanzisha timu na kuiendesha na leo inaonekana ni mkombozi wa soka la Mwanza.

Mkoa wenye kila historia nzuri kutokana na kuwa na timu bora za soka kama Pamba au wachezaji bora kabisa waliowahi kupita kama wale kutoka katika familia za akina Magongo, Maftaha na kadhalika.

Lakini kipindi cha miaka ya hivi karibuni, maisha ya majungu, kutopendana, kupaniana ili kufelishana ndiyo yaliyotawala mkoani Mwanza.

Mwanza wamekuwa watumwa wa Usimba na Uyanga badala ya kuwa mashabiki wa kutupwa wa Mbao FC na Toto African.

Tumeona msimu uliopita, mkoa wa Tanga ulipandisha timu tatu kwa pamoja na zote zikateremka daraja kutokana na majungu na chuki za wazi baina ya wao kwa wao.
Sasa ni Mwanza, nao hawapendani, wengi wana majungu, wengi hawatamani upande mwingine ufanikiwe na kwa kifupi ni watu ambao wamekuwa wakiangushana.

 Mbao FC, unaweza kusema ni kizazi kipya cha mabadiliko mapya ya mchezo wa soka katika mkoa wa Mwanza.
Ushindi wa Mbao FC jana unapaswa kuchukuliwa kama mapinduzi mapya katika soka katika Mkoa wa Mwanza.

Mbao FC imetuma ujumbe kwa Wanamwanza kwamba huu ni wakati wa kuungana na kuufanya Mkoa wa Mwanza urejee katika sifa yake.

Ukiangalia Mbao FC, imeingia fainali ikitumia wachezaji wa timu ya vijana chini ya miaka 20 wako wanne. Hii ni hazina ambayo watu wa Mwanza wanapaswa kuikuza, kuitunza na kuiendeleza.

Unaweza kusema wakati wa wapenda soka wa Mwanza kuacha majungu ambayo yamewaangusha na ndiyo maana umeona tokea kupotea kwa Pamba FC, Toto African imekuwa ni bingwa wa kuwania kuepuka kuteremka daraja.

Sasa Mbao FC inaonyesha ndani ya Mwanza kunaweza kukawa na vitu vingi na hasa vipaji ambavyo huwa haviendelezwi kutokana na watu kuwekeana chuki zaidi, kukwamishana na kupaniana.

Kwa kifupi Mwanza hampendi maendeleo yenu wenyewe, mmekuwa mkijikwamisha wenyewe na mmekuwa si watu mnaotaka mkoa wenu uendelee.

Mbao FC pamoja na viongozi wake wanastahili pongezi na sasa rudini, unganeni na muijenge Mwanza mpya kupitia ujumbe mpya wa Mbao FC ambayo imewafikishia ujumbe.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic