Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), imeingia mkataba wa miaka mitatu kuidhamini Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars wenye gharama ya shilingi bilioni 2.1 za Kitanzania.
Katika pesa hizo, Serengeti watakuwa wakiipa Taifa Stars shilingi milioni 700 kila mwaka, huku pesa zingine zikiongezeka kutokana na makubaliano waliyoafikiana wakati wa kutiliana saini mbele ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo, mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Helen Weesie, amesema: “Tunaona fahari kuiunga mkono Taifa Stars na tumeamua kuchukua fursa hii ya kuidhamini tukifahamu fika mchango unaotolewa katika sekta ya michezo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.”
Naye Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, aliishukuru kampuni hiyo kwa uungwaji mkono wake huku akisema kwamba itasaidia katika maandalizi ya timu hiyo kuelekea mechi za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) pamoja na ile inayowahusisha wachezaji wa ndani (Chan).
Ikumbukwe kuwa, hii ni mara ya pili kwa kampuni hiyo kuidhamini taifa Stars kwani mara ya kwanza iliingia mkataba wa udhamini kuanzia mwaka 2007 mpaka 2011.
0 COMMENTS:
Post a Comment