May 5, 2017
Na Saleh Ally
KARIBU kila mtu mzima kama ataambiwa anafanya mambo ya kitoto, basi atajisikia vibaya kwa kuwa wote tunajua namna ambavyo watoto wanavyoweza kufanya mambo ya kitoto.

Moja ya makosa makubwa ya watoto ni kutoelewa, kutojirekebisha na kutojua kubadili mambo kutokana na walichokiona au kujifunza!

Watoto wana uwezo mkubwa wa kurudia mambo au makosa yaleyale. Wakati mwingine wanakuwa na nafasi ndogo sana ya kujitambua, kujisoma au kubadili mambo hasa pale wanapoumia.

Wanapoumia, watoto hujirekebisha. Kama mtoto atagusa moto, ukamuunguza. Wakati mwingine ukimuambia, moto, utaungua basi mara moja utaona anaondoa mikono au mwili wake kwa hofu ya kuungua kwa kuwa tayari ameyajua makali ya moto.

Naanza kwa kujiuliza, Toto African, klabu ya soka mkoani Mwanza kwani wao hawawezi kuwa na hisia hata kidogo za wale watoto wenye ‘akili’ na kujifunza kutokana na kile ambacho kimewakuta misimu miwili mfululizo, kuwa wao ni watu wa kuepuka kuteremka daraja kila msimu.

Toto African, hawana uwezo wa kujifunza na kuachana na hisia au mipango ya hovyo kuwa na uwezo wa kupania mechi moja au mbili pekee katika msimu mzima na wakabaki kuwa na sifa ya kutofungwa na fulani?

Kikosi cha Toto African kilibaki kuwa kikosi chenye sifa kuu kwa Wanamwanza. Timu ambayo imebeba sifa ya Pamba ya Mwanza ambayo ilikuwa kiboko ya Simba, Yanga na timu nyingine yoyote ya Tanzania ambayo ilisafiri kwenda Mwanza, basi ilijua mbele yao kuna kazi.

Toto kwa misimu miwili mfululizo waliepuka kuteremka daraja, msimu wa tatu wakateremka. Wakapambana kwa misimu miwili wakafanikiwa kurejea tena Ligi Kuu Bara.

Baada ya kurejea, tayari wamecheza misimu miwili wakiwa katika hatihati ya kuteremka daraja na inaonekana hadi sasa hawana uhakika wa kuepuka kuteremka daraja kwa kuwa ni watu wa kunusurika karibu kila msimu.

Katika timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, kwa sasa Toto African iko katika nafasi ya 14, tayari katika zone ya kuteremka daraja. Ina pointi 26 sawa na Majimaji iliyo katika nafasi ya 15. Timu pekee inayozidiwa pointi na Toto African ni JKT Ruvu iliyo mkiani kabisa baada ya kukusanya pointi 23.

Mechi mkononi mwa Toto African ni nne. Nafasi yake ya kujaribu kusalimika ni kushinda zote na kitu kibaya zaidi, timu nne zilizo juu ya Toto zina pointi 30 na 31.

Maana yake hata kama moja itapoteza, Toto ikashinda itaendelea kubaki ilipo. Inaonekana hivi; ushindi wa mechi moja hauna msaada hata kidogo kwa Toto African.

Inategemea timu zipoteze mechi mbili nayo inatakiwa ishinde mbili ndipo inaweza kujikwamua katika tope ililonasa.

Toto imeendelea kufanya mambo ya kitoto kwa misimu mingi mfululizo na kila inapopanda Ligi Kuu Bara inamaliza ligi ikiwa “inapigania” roho yake kuhakikisha inabaki tena.

Jiulize wewe, viongozi wa Toto African ni watu wa namna gani? Watu wasiofikiri au kujifunza kutokana na makosa? Watu wa namna gani wasioumizwa na mabaya yaliyopita juu yao?

Nami najiuliza, wataacha lini kufanya mambo ya kitoto? Kwa nini siku moja Toto African isiweze kuingia katika mawazo ya “bwana mdogo” Mbao FC ambaye kapanda msimu huu na leo ana mawazo ya kuiwakilisha Tanzania kushiriki michuano ya kimataifa?
Mbao FC sasa ni wachanga, au kama ingekuwa umri ungewaita ni watoto lakini walio na mawazo ya kikubwa kwa kuwa wana malengo.

Toto African haijawahi kuwa hata na ndoto za kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho. Mbao FC walikuwa nayo ndiyo maana wamefika. Na sasa umefikia wakati wa viongozi wa Toto kuachana na mambo ya kitoto na kujifunza angalau kupitia hata Mbao FC ambao wanaweza kuyumba upande mmoja na kuonyesha wamejifunza kupitia mwingine.
SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV