May 6, 2017





BABA MZAZI WA DANI, DOMINGOES




Na Saleh Ally
MWANAMAMA Dona Lucia Ribiero alilazimika kupiga kelele mbele ya runinga yake kwa kusisitiza: “Usile, usile, acha kabisa usile”. Yalikuwa ni maneno ambayo alikuwa akijaribu kufikisha kwa mwanaye.


Dona Lucia asingependa kumuona mwanaye akila ndizi ambayo ilirushwa uwanjani na mashabiki wa soka ambao walikuwa wakionyesha ubaguzi wa wazi kabisa.

Hata hivyo, mwanaye huyo asingeweza kusikia sauti ya mama yake aliyekuwa akimuona kupitia runinga. Aliiokota na kuila ile ndizi.

Baadaye Dona Lucia alieleza kuwa hofu yake kubwa kwa mwanaye Dani Alves kula ile ndizi, huenda alihisi iliwekewa vitu vibaya vilivyolenga kumuumiza au kummaliza kabisa.

Kama mama lazima ana uchungu kwa mwana, lakini lazima afanye hivyo kwa kuwa Dani ndiye tegemeo la familia ya Domingos kwa sasa kwa kuwa wakati huo alikuwa akiichezea FC Barcelona ya Hispania, moja ya timu kubwa na maarufu kabisa duniani.

Familia ya Dani ambayo mama ni Dona Lucia ni moja ya mamilioni ya familia masikini kabisa nchini Brazil na duniani kote na wamekuwa wakitegemea kilimo cha vitunguu.


Wamekuwa wakitegemea kilimo katika ardhi kavu ya Jimbo la Bahia nchini Brazil. Baba yake mzazi aitwaye Sau Domingos alikuwa mmoja wa watu wenye nafuu ya maisha katika eneo hilo kwa kuwa aliweza kumiliki angalau trekta chakavu.

Domingos amejaaliwa kupata watoto watano, Dani akiwa mmoja wao na watatu walikuwa wakicheza mpira huku Dani akionekana ndiye alikuwa na uwezo mdogo kuliko wenzake.
Waliishi maisha magumu sana na wakati mwingine ya kushindia mkate kwa siku nzima wakisubiri kula usiku ambacho waliamini ni chakula muhimu.

Wakati kila mmoja amekula mkate tu, lakini walikuwa wakiendelea na kilimo katika joto kali la nyuzijoto 40 huku ardhi ikiwa kavu kupindukia lakini hakuna aliyelaumu badala yake ilikuwa ni kufanikisha lengo la kilimo.

Mara kadhaa kaka yake Dani alilalamika mdogo wake alikuwa hafai kucheza soka, huenda angebaki nyumbani kusaidiana na baba yake kuhusiana na kilimo.

Hata hivyo, Dani hakukubali, maana ndoto yake ilikuwa ni kubadilisha maisha ya familia yake atakapojitegemea. Kila aliporejea nyumbani saa 11 jioni, pamoja na kushindia mkate na kushinda akifanya kazi, lakini hakukubali, alichukua mpira wake na kwenda mazoezini.

MAMA MZAZI WA DANI

Baada ya kaka yake kuona Dani ameshindikana au hazuiliki, aliamua kumshawishi kurejea kucheza beki wa kulia kuliko kubaki kama mshambulizi kwa kuwa pamoja na kucheza vizuri, alifikisha miezi mitatu bila kufunga hata bao moja, kwao halikuwa jambo sahihi.

Timu yao ya kijiji ilikuwa ni Bahia FC, kaka yake alikuwa tegemeo lakini Dani alionekana ni msaada zaidi baada ya kukubali kuanza kucheza beki na rasmi mwaka 2001 alisajiliwa kwenye timu ya wakubwa na kufanikiwa kufunga mabao mawili.

NYUMBANI KWAO
Msimu mmoja tu ulimtosha Dani kuondoka Bahia na kujiunga na Valencia ya Hispania ambayo nayo aliichezea misimu mitano tokea 2002 hadi 2008 alipotua FC Barcelona ambayo ilitangaza kumpa mshahara wa jumla ya pauni milioni 5 kwa mwaka.

Kwa sasa Dani ndiyo picha iliyobeba matumaini ya watu wa Bahia kwamba katika ulimwengu huu hakuna linaloshindikana.

Dani aliyekuwa akilala katika chumba cha hali ya chini, chumba ambacho zikinyesha mvua kubwa walilazimika usiku kukinga maji kutokana na bati kuwa na matobo, sasa si yule tena.

Dani ambaye kwao kulikuwa na runinga ya kichogo, ndogo na wakati mwingine waligombana kwa kila mtu kutaka kuangalia chaneli tofauti, ndiye aliyebadilisha maisha ya familia ya Domingos.

Beki huyo sasa yuko Juventus na ameonyesha msaada mkubwa na kuisaidia timu hiyo kuing’oa Barcelona katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mechi ya kwanza ya nusu fainali, Dani ametoa pasi mbili ambazo zote zilizaa mabao mawili yaliyofungwa na Higuan na kuipa Juventus ushindi wa 2-0 dhidi ya AS Monaco ambayo itasafiri kwenda Italia katika mechi ya pili.

Dani ameijengea familia yake nyumba mpya, kubwa na yenye bwawa la kuogelea. Amemnunulia baba yake matrekta matatu mapya, gari la kubeba mizigo yake ikiwa ni pamoja na kulijenga upya kanisa la kijijini kwao ambalo lilikuwa na muonekano chakavu unaotia huruma.

Watoto wengi katika eneo hilo, walizidi kuhamasika baada ya Dani kuitwa kwa mara ya kwanza kucheza katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil ambalo kwa utamaduni wa Wabrazili ni jambo kubwa sana kwa mtu anayefanikiwa kuichezea timu hiyo.

Kocha Luiz Felipe Scolari alikuwa wa kwanza kumuita na baba yake alichanganyikiwa. Kwa kuwa wakati akikua, Dani hakuwahi kuwaza kucheza soka nje ya Brazil na zaidi aliwaza mafanikio huku akiamini kama atafikia kucheza timu kama Santos, kwake lingekuwa jambo kubwa sana.

DANI ALVES AKIWA NA SALEH ALLY JEMBE

Katika maisha yake, hakuwahi kusafiri kwenda mjini au katika miji mikubwa kama Sao Paulo au Rio de Janeiro. Ndiyo maana anapenda kujiita “Mbuzi wa Kijijini” akiwa na maana mtu kutoka kijijini asiye na makuu.

Sasa ana kila anachotaka katika maisha yake, nyumba na magari mazuri lakini ambacho ameahidi ni siku moja kurejea na kumalizia soka lake nchini Brazil na kucheza katika klabu mojawapo kubwa ili kutimiza ndoto.

Kinachovutia kwa Dani anaonekana alipania kuisaidia familia yake zaidi hata kuliko kujulikana. Alitaka kufanikiwa na kupata ili awasaidie wazazi wake.

Hii inaonyesha kutaka mafanikio kwanza badala ya kutaka fedha kwanza kunaweza kuwa msaada. Ndoto yake ilikuwa ni kuwa mkombozi, ndiyo maana hakukubali alipozuiwa.

KANISA LA KIJIJI

Kaka yake aliona hakuwa na kipaji sahihi na alisumbuka tu, bora abaki nyumbani. Yeye akajiamini, akaweka msisitizo na kujiamini atafanya vizuri huku akiamini atakuwa msaada au mkombozi kwa kuwa waliishi maisha ya kupindukia.

Ukiachana na kuisaidia familia yake, ndugu zake wote amewapa mtaji na wanaendesha maisha yao vizuri lakini hata baada ya miaka 30 kwa kuwa sasa ana 33, Dani anaendelea kuonekana kama ndiyo kinda kwani kiwango chake kipo juu.

Kumbukumbu ya maisha magumu ya zamani inaweza kuwa changamoto ya kuendelea kupambana kufanya vizuri. Ukimuona Dani anajituma uwanjani, basi nawe ujitume pia, usisahau maisha magumu ya kwenu Shinyanga, Mbeya, Sumbawanga, Kigoma na kwingineko kwa kuwa ugumu wa maisha pia ni sehemu ya msukumo wa kutaka mabadiliko.


Usione wachezaji waliofanikiwa kifedha ukadhani wametokea katika hali nzuri. Wengi wamekuwa na maisha magumu ndiyo maana hawakuchoka. Vipi wewe unachoka wakati kwenu ni kama kwa kina Dani?

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic