May 6, 2017Haina ubishi tena kwa kuwa Simba wao wenyewe kwamba watakuwa na mechi ngumu na wanataka kushinda dhidi ya African Lyon, kesho.

Simba wanataka kushinda kwa ajili ya umuhimu wa pointi tatu kwa ajili ya ubingwa lakini pia kulipa kisasi.

Kama unakumbuka Simba walifungwa bao 1-0 na African Lyon katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, kesho timu hizo zinarudiana na Wekundu wa Msimbazi, wamesema Lyon wakijichanganya kidogo tu itakula kwao.

Februari mwaka huu, Lyon iliifunga Simba bao la jioni lililofungwa na Abdallah Mguhi na kutibua rekodi ya Simba ya kutopoteza mechi iliyokuwanayo wakati huo.

Hadi sasa Simba ipo kileleni mwa ligi kuu ikiwa na pointi 59 ikifuatiwa na Yanga yenye 56 lakini Wekundu wa Msimbazi wana mechi tatu zilizobaki wakati Wanajangwani wanazo tano.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema, Lyon ni timu nzuri inayoweza kupata matokeo dhidi yao lakini ikiingia uwanjani na kudhani Simba waliyoifunga ni sawa na watakayokutana nayo basi itakula kwao.

“Tumejiandaa vizuri na mchezo huu, na Lyon wakidhani wanacheza na Simba ile waliyoifunga basi tutawafunga kwani sasa tupo vizuri na bado tunawania ubingwa wa ligi kuu licha ya michezo michache tuliyonayo,” alisema Mayanja.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog yeye alisema mechi hiyo itakuwa ngumu sana kwao lakini wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

“Tunaiheshimu African Lyon kama moja ya timu bora katika ligi, hawa walitufunga katika mzunguko wa kwanza hivyo na sisi tunataka tuwafunge sasa,” alisema Omog.

Lyon inanolewa na Kocha George Otieno ambaye hivi karibuni alisema watahakikisha wanapambana katika mechi zao zilizobaki ili waweze kubaki kwenye ligi.
Lyon ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 31 ikiwa na michezo 27, hivyo ipo katika hatari ya kushuka daraja.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV