June 11, 2017



Na Saleh Ally
KATIKA soka nchini, kuna mambo mengi ambayo ni siri na yamekuwa yakiendelea kimyakimya huku yakipewa nafasi kubwa ya usiri.

Ni vigumu wengi kukubali kwamba suala la hongo limekuwa likifanyika. Unajua hatari yake na wanajua iwapo watabainika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Wako wanaofanya na kuna wachezaji wamekuwa wakichukua hongo kuzisaidia timu fulani.

Kuna wachezaji wamekuwa wakicheza chini ya viwango kwa lengo la kuzisaidia timu nyingine zifanye vizuri zaidi.

Ninaamini kwa wanasoka mnaosoma makala haya sasa utakubaliana nami kuhusiana na upuuzi huu ambao umekuwa ukiendelea kuudidimiza mchezo wa soka nchini.

Kwa kuwa mambo hayo yapo, wako ambao wamekuwa wakiingizwa kwenye mkumbo kutokana na kufanya makosa ya kweli ya kimpira.

Tukubaliane, wako ambao wamekuwa wakifanya upuuzi huo halafu wanaahidiwa kwamba mwishoni mwa msimu, watasajiliwa na timu husika.

Unapofikia wakati wa usajili, viongozi wamekuwa wakiwakimbia kwa kuwa wanaamini hivi sasa kuwa kama wao waliwashawishi kufanya jambo kuhujumu timu walizokuwa wanazitumikia basi itakuwa rahisi kuzihujumu na zao kama wakiwasajili.

Wachezaji ambao umepata ajira katika klabu fulani, halafu anatokea mtu, anakushawishi kuiangusha timu inayokulipa mshahara ili upate posho ya usaliti na ukakubali, basi wewe ni poyoyo hasa usiyejielewa.

Wachezaji wenye tabia hizo wamebandikwa majina ya “duka” au “maduka”. Maana yake “wanauza” mechi.

Ajabu hawajaisha na wanaendelea kuwepo, na hii inaonyesha kiasi gani wachezaji wengi hawajitambui.

Kinachoshangaza zaidi, wakati wa usajili, viongozi hujadili kuhusiana na wachezaji “maduka” wakihofia kuwasajili na wangependa wasajiliwe kwingine ili baadaye wawasaidie.


Wachezaji amkeni, vizuri kutengeneza imani ya uwanjani, nje ya uwanja na maisha yanayofuata weledi. Acheni tamaa za kipuuzi zinazowafanya muwe “maduka” yanayokimbiwa na wanaosababisha muwe maduka.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic