June 11, 2017



Na Saleh Ally
MWAKA 2014, Diego da Silva Costa alijiunga na Chelsea akitokea Atletico Madrid ya Hispania. Sasa ni misimu mitatu na tayari amebeba makombe matatu akiwa na klabu hiyo ya London, England.

Amebeba ubingwa wa Ligi Kuu England, mara mbili. Pia mara moja ubingwa wa Kombe la Ligi.

Costa asili yake ni Brazil, mara nyingi nimekuwa nikijiuliza kwamba wakati anazaliwa mimi ndiyo nilikuwa nimeanza shule ya msingi? Maana amezaliwa 1988. Aah! Wakati napotezea kwa kuwa naona si ishu ya msingi sana.

Lakini nimekuwa nikivutiwa na utukutu wake kama mshambulizi ingawa wakati mwingine huwa unazidi, maana jamaa, inakuwa zaidi ya baunsa.

Ukisema kuhusiana na mchango wake katika kikosi cha Chelsea, hakuna ubishi ni mkubwa na amekuwa akiifanya kazi yake vizuri.



Ndiyo maana ndani ya misimu mitatu, ameweza kuisaidia Chelsea kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England mara mbili, pia Kombe la Ligi, si kitu kidogo hata kidogo.

Katika mechi 87 akiwa na Chelsea, amefunga mabao 52, hizi ni takwimu zinazothibitisha kwamba Costa ni mshambulizi bora kabisa.

Hivi karibuni, Costa ametoa siri hadharani kwamba huu ni msimu wake wa mwisho na Chelsea kwa kuwa tayari ametumiwa ujumbe mfupi wa maneno na kocha wake, Antonio Conte ukimueleza kwamba hamhitaji tena.

Conte amefanya mambo kama mswahili fulani hivi, unaweza kujiuliza hivi kweli alishindwa hata kumpigia simu mtu kama Costa na kumueleza uamuzi wake?

Kuna taarifa kwamba Conte anamhitaji Romelu Lukaku kutoka Everton. Yuko sahihi kwa kuwa Lukaku amefunga mabao mengi zaidi ya Costa ingawa Costa ameisaidia timu yake kubeba ubingwa.

Takwimu zinaonyesha msimu uliopita, Costa amecheza mechi 42, kafunga jumla ya mabao 22 na kutoa asisti saba. Wakati Lukaku amecheza mechi 37, kafunga mabao 25 na kutia asisti sita.

Kwa maana ya faida kwenye timu hawa ni wachezaji wanaofanana sana, lakini jiulize uwamuzi wa Chelsea una faida gani?

Hakika alichofanya Conte kwa Costa kimeonekana kuwashangaza watu wengi. Inawezekana halikuwa ni jambo sahihi kwa maana ya mchango wa Costa ambavyo umekuwa, alistahili heshima.

Kama barua ilishindikana kama upande wa klabu, angeweza kupigiwa simu na Conte, huenda lingekuwa jambo jema.

Watabiri wa mambo wameanza kuzungumzia suala la Everton kuipandishia bei Chelsea, kwamba huenda itataka Lukaku sasa auzwe kwa pauni milioni 100, wakati kama ni dau kubwa sana Chelsea huenda ingetoa pauni milioni 80 ambazo inaamini ziko juu sana pia ni saizi ya Mbelgiji huyo aliyewahi kukipiga Chelsea kabla ya Kocha Jose Mourinho kumuacha aende.

Ukiachana na “Uswahili” wa Conte, ndani ya Costa kumekuwa na shida. Utukutu na kumekuwa na malalamiko ya ustaarabu na namna ya kuishi na wenzake.

Klabu zinatofautiana na makocha pia wanatofautiana, huyu anapenda hiki na huyu anapenda kile. Inawezekana Conte hafurahishwi na tabia za kijeuri za Conte.

Kuna ule mfumo wa maisha ya mwanadamu ambao unaeleza namna ambavyo watu wengi wenye vipaji, akili au fedha nyingi wamekuwa wakifeli kutokana na tabia zao kuwa mbaya.

Tabia ya Costa si sahihi, ujeuri au kuanzisha ugomvi sehemu ambayo si sahihi. Kulazimisha ugomvi au kulazimisha dharau wakati soka si ugomvi, ni ushindani na unasisitizwa uwe ushindani ‘fair’.

Wako ambao wamekuwa wakikerwa na Costa wanasema na wengine wamekaa kimya. Huenda Conte amekerwa kupindukia na ameshindwa kujizuia.

Au inawezekana Conte hakukerwa sana lakini kuna mabosi wake wamekerwa zaidi, kupitia yeye wameamua kuchukua hatua hiyo lakini namna ya kuifikisha ikawa shida.


Hili suala la Costa na Conte, linaweza kuwa funzo kwamba ubora wa mtu hautengenezwi na kitu kimoja tu. Vizuri kuutengeneza ubora wako katika wigo mpana na nidhamu inayojenga ubinadamu inaendelea kubaki namba moja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic