Na Saleh Ally
JULAI 2 ndiyo itakuwa fainali ya michuano ya Mabara, maarufu kama Confederation Cup ambayo inaanza kutimua vumbi rasmi jijini Saint Petersburg, Urusi, Jumamosi hii.
Michuano hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Kombe la Dunia na inawakutanisha vinara au Mabingwa wa Mabara ili kutafuta mbabe wao.
Kwa hapa nyumbani, mashabiki wa soka nchini watafaidika kuiangalia michuano hiyo kupitia King’amuzi cha StarTimes ambacho kitaonyesha michuano hiyo kuanzia mechi ya kwanza hadi fainali, mubashara kabisa.
Michuano ya Mabara ina makundi mawili yenye timu nane, maana yake Kundi A lina timu nne na nne nyingine Kundi B. Kwa kuangalia haraka, unaona haitakuwa michuano rahisi hata kidogo.
Wanakutana wababe pamoja na mwenyeji Urusi ambaye atataka kubakiza heshima nyumbani kabla ya michuano ya Kombe la Dunia inayofanyika nchini mwake mwaka 2018.
Lakini bingwa wa Ulaya ni Ureno, inayoongozwa na mwanasoka bora duniani, Cristiano Ronaldo ambaye yuko katika kiwango bora kabisa.
Hakika Ronaldo kama mchezaji bora atakuwa anataka heshima kubwa ya kuhakikisha anafanya vizuri na kuendelea kuonyesha ni mchezaji muhimu katika kikosi chake cha Real Madrid pamoja na timu ya taifa ya Ureno ambayo yeye ni nahodha.
Kundi A lina wenyeji Urusi, New Zealand, Mexico na Ureno. Utaona kuna timu mbili za Ulaya ambako soka ni la kiwango cha juu, halafu Mexico ambayo inajulikana kwa uwezo wake pamoja na kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kubadili matokeo.
Ureno wana Ronaldo na wachezaji ambao walionyesha uwezo mkubwa wakibeba ubingwa wa Ulaya na kikosi cha kocha Fernando Santos hakina mabadiliko makubwa.
Unaweza kuwadharau New Zealand lakini unapaswa kukumbuka kuwa katika kila michuano mikubwa kama hiyo kunakuwa na “Surprise”, huenda inaweza kutoka kwa mchezaji ambaye hakutarajiwa au timu ambayo haikutegemewa itafanya hivyo.
Kundi B, Ujerumani ndiyo mabingwa wa dunia, kiwango chao hata kama kimeonekana kulega kidogo lakini wanapoingia katika michuano kama hiyo, vijana wa kocha Joachim Loew hawataki mchezo.
Ujerumani wanapewa nafasi ya kufika fainali au kuchukua ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwa ni kikosi kilichokaa pamoja kwa zaidi ya miaka mitano na mabadiliko ni madogo sana.
Lakini angalia Cameroon, mabingwa hawa wa Afrika ambao walishangaza wengi ambao hata katika fainali ya Kombe la Mataifa Afrika kule Gabon, hakuna aliyetarajia wangeonyesha soka safi na mwisho kuwa mabingwa.
Cameroon ina wachezaji wengi vijana, Simba hao wasiofungika wanajulikana kwa kutumia nguvu lakini kasi ya viungo na washambulizi wake inawapa hofu Chile, Australia na hata Ujerumani.
Chile wanatokea Amerika Kusini, sehemu ambayo ina soka la urembo zaidi na vipaji zaidi vya soka kuliko sehemu nyingine yoyote duniani.
Kumbuka kama Ureno watashinda ubingwa wa Kombe la Mabara, maana yake wao ni bora zaidi hata kuliko Argentina inayoongozwa na Lionel Messi na Brazil ya Neymar. Hivyo hakuna ubishi kwamba watatoa ushindani mkubwa na wana nafasi ya kusonga mbele.
Katika kundi hili la B, Australia ndiye anaonekana kama kibonde. Lakini anaingia kwenye ile “Surprise”, chochote kinaweza kutokea na imekuwa ni kawaida. Hivyo lolote wanaweza kufanya la kushangaza.
Kwa kuwa StarTimes wataonyesha kupitia king’amuzi chao na Watanzania wengi wapenda soka wana uwezo wa kuona kwa kuwa kampuni hiyo imesambaa maeneo mengi nchini kutokana na bei yao kuwa nafuu, basi itakuwa nafasi nzuri kwa wapenda soka kupata burudani murua na mubashara kabisa.
KUNDI A
Urusi
New Zealand
Ureno
Mexico
KUNDI B
Cameroon
Chile
Australia
Ujerumani
RATIBA:
KUNDI A
Juni 17 Urusi Vs New Zealand
Juni 18 Ureno Vs Mexico
Kundi B
Juni 18 Cameroon Vs Chile
0 COMMENTS:
Post a Comment