June 7, 2017




Michuano ya SportPesa Super Cup imeendelea kutikisa jiji la Dar es Salaam na viunga vyake kwa kuikutanisha miamba ya soka ukanda wa Afrika Mashariki kutoka nchini Kenya na Tanzania.

Mpaka sasa mechi nne zimeshachezwa kwenye michuano hiyo ambayo imeanzia moja kwa moja kwenye hatua ya mtoano ya robo fainali kwa timu kutoka Kenya kupambana na wenzao kutoka Tanzania.

Kwa siku mbili mfululizo tumeshuhudia soka la kuvutia kutoka kwa vilabu vyote viwili huku upinzani ukiwa ni mkubwa zaidi tofauti na ilivyotarajiwa huku wale ambao walichukuliwa kama vibonde kabla ya kuanza kwa mashindano haya, wakiwashangaza wengi.

Vilabu vya AFC Leopards, Yanga, Gor Mahia na Nakuru All Stars vimeshatinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha kuipata timu moja tu itakayomenyana na Everton kwenye mchezo utakaopigwa Julai 13 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Huku mechi za nusu fainali zilitarajiwa kuanza kutimua vumbi hapo kesho, yafuatayo ndiyo mambo makuu unayotakiwa kuyajua kuhusiana na michezo iliyopita ya robo fainali;

GOR MAHIA

Gor Mahia
Gor Mahia ndio timu pekee iliyotinga hatua ya nusu fainali ya SportPesa Super Cup kwa ushindi wa kawaida ndani ya dakika 90 ambapo waliweza kuwafunga Jang’ombe Boys kwa mabao mawili yaliyofungwa na mshambuliaji Medie Kagere.

Changamoto ya Mikwaju ya Penati
Kutokana na mashindano hayo ya SportPesa Super Cup kuanzia katika hatua ya mtoano, ilikuwa ni lazima timu moja iage mashindano na nyingine itinge katika hatua inayofuata ya nusu fainali.

Mechi tatu miongoni mwa nne zilizochezwa kwenye hatua ya robo fainali ziliamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika kwa sare.

Mechi ya kwanza kati ya Singida United na AFC Leopards iliamuliwa kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1 na AFC Leopard kushinda kwa jumla ya mikwaju 5-4.

Mechi ya pili kati ya Yanga na Tusker pia iliamuliwa kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare tasa ya kutofungana na kuishuhudia Yanga ikitinga nusu fainali kwa jumla ya penati 4-2.

Na pia mechi kati ya Simba na Nakuru All Stars iliyopigwa siku ya Jumanne iliamuliwa kwa mikwaju ya penati 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare tasa.

Medie Kagere
Mshambuliaji wa Gor Mahia ya Kenya, Medie Kagere ndiye mchezaji anayeongoza kwa upachikaji mabao hadi kufikia sasa baada ya kuweka kimiani mabao mawili kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Jang’ombe Boys uliopigwa siku ya Jumanne kwenye uwanja wa uhuru kuanzia majira ya saa nane kamili mchana.

Kagere raia wa Rwanda alifunga mabao yote mawili katika kipindi cha pili huku bao la pili likiwa ni la mkwaju wa panati kufuatia beki wa Jang’ombe Boys kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.


Mikwaju ya penati.
Jumla ya mikwaju ya penati 29 imepigwa kwenye hatua ya robo fainali ya SportPesa Super Cup ambapo 28 kati ya hiyo ilipigwa nje ya dakika 90 huku mkwaju mmoja ukipigwa ndani ya dakika 90.
Katika penati 29 zilizopigwa, 25 kati ya hizo ziliweza kutinga wavuni ambazo ni sawa na asilimia 86.2% huku panati nne (4) zikishindwa kutinga wavuni ambazo ni sawa na asilimia 13.7%.
Golikipa wa Yanga, Deogratius Munishi ndiye golikipa pekee aliyeweza kuokoa mchomo wa penati miongoni mwa penati nne zilizokoswa kwenye mashindano hayo huku nyingine mbili zikiota mbawa na nyingine moja ikigonga nguzo.


Yanga
Yanga ndiyo timu pekee kwa upande wa Tanzania iliyotinga hatua ya nusu fainali baada ya kuwafungasha virago mabingwa wa Kenya, Tusker FC.
Timu za Simba, Singida United na Jang’ombe Boys zimeshindwa kufurukuta mbele ya timu tatu za Kenya za Nakuru All Stars, Gor Mahia na AFC Leopards ambazo zimetinga nusu fainali.


Kuelekea Nusu Fainali
Baada ya mapumziko ya siku moja, burudani itaendelea siku ya Alhamisi kwa michezo miwili ya nusu fainali ambapo mchezo wa kwanza utapigwa majira ya Saa nane kamili mchana kati ya mabingwa wa Tanzania bara, Yanga watakaopambana na AFC Leopards kutoka Kenya huku mchezo wa pili ukianza saa kumi na robo alasiri kati ya Gor Mahia na Nakuru All Stars.
Tukutane Uwanja wa Uhuru!


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic