June 24, 2017MAYAY 

Na Saleh Ally
KITAALUMA Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Giovanni Infantino ni Sports Administrator, yaani mtaalamu wa utawala wa michezo.

Infantino ambaye jina lake la utani ni Gianni hakuwahi kucheza soka na kuwa nyota wa timu yoyote maarufu ingawa anajulikana kuwa ni shabiki mkubwa wa Inter Milan ya Italia.

Rais huyo wa Fifa ni raia wa nchi mbili, Italia na Uswiss na ndiye kiongozi mkubwa zaidi katika anga za michezo baada ya kuichukua nafasi hiyo kutoka kwa Sepp Blatter.


MTEMI
Kitaaluma Blatter aliyeiongoza Fifa kwa miaka 17 pia amesomea utawala wa masuala ya michezo kama ilivyo kwa Infantino. Hakuwahi kucheza soka kwa kiwango cha juu na kuwa tegemeo au maarufu kama ilivyo kwa Cristiano Ronaldo au Lionel Messi au maradufu nchini ya hapo.

Blatter aliwahi kuwa Ofisa Mawasiliano ya Bodi ya Utalii eneo la Canton, lakini baadaye akawa kiongozi wa mpira wa magongo na aliingia Fifa kupitia mchezo huo akiwa anashughulikia Michezo ya Olimpiki.

Ninaweza kukumbuka wengi sana hawakuwahi kucheza soka wakawa viongozi wazuri wa mchezo wa soka. Bado ninaweza kukumbusha makocha wengi kama ilivyo kwa Jose Mourinho au Arsene Wenger kuwa hawakupata mafanikio katika soka na kuwa maarufu lakini walifanya vizuri katika uongozi.Alipofikia Infantino, maana yake amepita hatua kwa hatua hadi yupo alipo. Kila alipoaminika ndipo alipozidi kupanda. Sasa anaweza kuaminika zaidi na kufanya vizuri.

Uongozi ni kipaji pia, kusomea ni jambo muhimu kabisa. Kuongoza mpira, nataka kuweka msisitizo si lazima uwe umecheza maana wako waliowahi kucheza wakafeli katika uongozi na wako waliweza lakini wako ambao hawakuwahi kucheza kweli walifeli na wengine walifanikiwa.

Jambo zuri katika suala la uongozi kwanza ni sera na kuangalia nyuma huyu mtu anaweza akafanya nini. Anapokuwa anazungumza kwa kuwa mgombea ni anayejulikana ni rahisi kujua anachosema ni sahihi au la.

Katika uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao umepangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma, baadhi ya waliojitokeza kugombea tena katika nafasi zote za juu na zile za chini wako wachezaji wastaafu wa soka.

SHIJA

Katika Urais, amejitokeza Ally Mayay ‘Tembele’, makamu rais yuko Mtemi Ramadhani na wajumbe kuna Leopold Mukebezi, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Bakari Malima.

Nianze kwa kuwapongeza watu hawa kwa kuwa wameonyesha uthubutu tofauti na wachezaji wengi ambao wamekuwa waoga.

Kama ni maoni yangu, nitakuambia wanastahili kupata kura lakini suala la kushinda, hili siwezi kuliwekea uhakika kwa kuwa lazima kuwe na nafasi ya wao kuwaeleza wapiga kura nini waliufanyia mpira wa Tanzania na kipi watafanya wakipewa nafasi.

MWAKALEBELA

Mimi nataka nitofautiane na wachezaji wote wa zamani kwamba, kigezo cha “sisi tuna uchungu wa mpira” kwa kuwa mlicheza, haiwezi kuwa kigezo cha nyie kupewa kura.

Mpira mna uchungu nao, kipindi hicho ilikuwa ni kazi yenu na uliwaingizia fedha na kuendesha maisha, lakini bado kuna sehemu ambazo tunaweza kusema hamkufanya vizuri, hivyo mnaweza kuutumia katika kampeni zetu mfano wa kuwa mlicheza lakini hauwezi kuwa kila kitu.

Wekeni sera zenu na elezeni walipokosea na nini cha kufanya. Sioni kama sawasawa kama wagombea watapigiwa kura na kushinda kwa kigezo cha kuwa walicheza mpira tu huku tunajua watakaposhinda nafasi ya urais, makamu rais au ujumbe hawatakuwa wakicheza mpira huko.

WAMBURA

Badala yake watakuwa wakiongoza na njia za uongozi zilivyo si kupiga danadana wala kukimbia uwanjani. Badala yake ni mambo tofauti kabisa ingawa kweli kama ulicheza, itakusaidia katika kazi.

Wote niliowataja si wageni kwangu, nimeshirikiana nao mara moja au mbili kikazi. Ni watu wanaojitambua na uwezo wa kufanya mambo yao vizuri kabisa. Kuhusiana na uongozi, ninaamini wanaweza kufanya jambo.

Niweke msisitizo, kucheza mpira pekee hakiwezi kuwa kigezo bora kimoja tu cha mtu kupewa kuongoza mchezo wa mpira katika kiwango cha shirikisho.

Naamini itakuwa vema wakamwaga sera za uhakika na hiyo ya kucheza mpira iwe sehemu ya chagizo kwa kuwa inajulikana. Ninaamini wanaweza kuwa na nafasi ya kusaidia kwa kuwa tayari wana mfano kwa kuwa Leodegar Tenga aliyefanya vizuri zaidi hata kuliko Jamal Malinzi aliyepo sasa.


Sasa basi, wajipange kwa sera na mipango inayoingia na kushawishi masikio ya wapiga kura na wasio wapiga kura kulingana na walichokipanga kutoka kwenye tope tulilokwamba na si kung’ang’ania tu, “nilicheza mpira, nina uchungu nao.”

2 COMMENTS:

  1. Mpira sio siasa sera tunataka pia,mtu anaejua mpira nini na unataka nini,watakuja watu na sera za kuwanufaisha wajumbe,wakachaguliwa

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV