July 5, 2017Mkurugenzi Mkuu wa Klabu ya Everton inayotamba kwenye Ligi Kuu England, Robert Elstone, anatarajia kuongoza semina kwa viongozi wa klabu za soka nchini, zikiwemo Simba na Yanga, itakayofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Semina hiyo itafanyika kabla ya mchezo kati ya Everton na bingwa wa SportPesa Super Cup, Gor Mahia ya Kenya, itakayochezwa Julai 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Itakuwa ni semina ya kuwajengea uwezo wa kuongoza, viongozi wa soka nchini na wataalamu wa benchi la ufundi.
Mapema mwezi uliopita, Robert Elstone pamoja na nguli wa zamani wa klabu hiyo, Leon Osman ambaye kwa sasa ni balozi wa klabu hiyo, walitembelea Tanzania kwa ajili ya kutoa taarifa rasmi juu ya ujio wao nchini.

Bosi huyo anataka kuwafunda viongozi kuhusu uendeshaji wa klabu ya mpira wa miguu kibiashara, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa mashabiki katika soka.

“Kwenye nadharia nzima ya masoko katika mpira wa miguu, kuna vitu viwili vikuu ambavyo Everton imekuwa ikivitilia mkazo kwa miaka mingi. Moja ni kuongeza mashabiki wetu, na pili ni kujenga hali ya uaminifu kwa mashabiki wetu.


“Tunathamini sana uaminifu wa mashabiki kwa klabu katika masoko ya mpira wa miguu na mpango kazi wetu mkubwa ni kuingiza mashabiki wapya kwenye mtandao wetu na kuhakikisha kuwa tunabaki na mashabiki hao kwa muda mrefu,” alisisitiza Elstone.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV