July 8, 2017




Na Saleh Ally
 UNAWEZA kuanza kuona kama vile Arsene Wenger amezidiwa na sasa hana ujanja zaidi ya kufanya jambo moja, kubadilika kutoka alichoamini hadi kufanya wanachoamini.

Awali, Wenger ndiye aliaminika kuwa kocha mbahili au mchumi kuliko wote duniani linapofikia suala la kununua wachezaji kutoka timu moja kwenda Arsenal.

Alikuwa na tabia ya ukarabati, anachofanya ni kuangalia mchezaji anayemuona ni bora lakini “amechoka”, yeye anamchukua na “kumtengeneza” na baadaye kuwa bora.
 Mfano mzuri ni Denis Bergkamp kutoka Inter Milan na Thierry Henry kutoka Juventus ambako walionekana kama wamepoteza matumaini.
 Kwa kuwa njia hiyo ilifanya vema, Wenger akakomaa nayo hadi baadaye mambo yalipoonekana kuwa magumu muda wote. Msimu uliopita, nafuu pekee ya yeye kubaki Arsenal ilionekana ni ubingwa wa Kombe la FA na sasa suala la usajili, ameona kama litamchongea.

Usajili wake wa kwanza kwa mshambuliaji ni pauni milioni 52.6 (Sh bilioni 150.8) akivunja rekodi ya usajili Arsenal kwa kumsajili mshambulizi Alexandre Lacazette kutoka Lyon ya Ufaransa.

Utakumbuka miaka miwili na ushee iliyopita, presha ilipokuwa kubwa alilazimika kuiziba kwa kulipa pauni milioni 42.4 (Sh bilioni 121.6) akimsajili Mesut Ozil kutoka Real Madrid.

Imani yake kubwa kwa Olivier Giroud ingekuwa vigumu sana kumsajili Lacazette. Lakini hali ilivyo, presha imemzidi na kumfanya akubali kubadilika, sasa ameamua kusajili zaidi na anaonekana kuweka nguvu nyingi katika ushambulizi.

Kufanya hivyo ni jambo jema ingawa kwa harakaharaka unaweza kusema Wenger amepasahau nyuma. Safu yake ya ulinzi haikuwa na ubora wa juu na huenda ilihitaji kuimarishwa zaidi kwa kupata beki mwingine imara kwelikweli ambaye atakuwa kiongozi kama ilivyo kwa Laurent Koscielny.

Ukiangalia takwimu za msimu uliopita, katika mechi 38, Arsenal ilifungwa mabao 44 na kufunga 77. Ikawa imeshika nafasi ya tano katika ligi na nafasi ya tano kwa mabao ya kufunga.

Lakini kwa maana ya difensi bora, Arsenal ilishika nafasi ya sita baada ya Tottenham, Chelsea, Man United, Man City na Liverpool.

Ukweli ni kwamba hajapasahau ndiyo maana moja kwa moja ameamua kumsajili Sead Kolasinac kutoka Schalke 04 ya Ujerumani na huyu anaonekana atakuwa mpinzani wa Kieran Gibbs na Nacho Monreal.

Ingekuwa ni ushauri wangu, ningesisitiza kwa Wenger kuwa anahitaji mtu wa shoka zaidi wa kati ambaye pamoja na kuwa mchezaji atakuwa kiongozi hasa.

Bahati nzuri kwa kipa Petr Cech, Wenger anakuwa na uhakika zaidi na ndiyo maana kuhakikisha makipa wanakuwa juu zaidi ameamua kumchukua kipa wake wa zamani, Jens Lehmann kuwa kocha wa kikosi cha kwanza.

Wenger ameona kuwa Arsenal ilikuwa na nafasi ya kuwa bingwa baada ya mechi 15 za awali, ikawa na nafasi hiyo hadi mechi 18 baadaye lakini baada ya hapo ikaanza kuporomoka hadi ikawa timu ya kuwania kucheza Top Four.

Kumbuka msimu mmoja kabla, Arsenal ilikuwa namba moja katika nafasi ya kubeba taji kwa kuwa vigogo wote kama Chelsea, Manchester United, Liverpool na hata Man City walikuwa wamepotea. Ubingwa ukachukuliwa na Leicester City.

Baada ya vigogo wenzake kukaa vizuri, inaonekana mambo yamezidi kuwa magumu zaidi na Arsenal imeangukia nje ya Top Four.

Tayari Wenger amekuwa ni mtu ambaye hana ujanja. Kamanda ambaye ameamua kunyoosha mikono huenda kufanya asichokiamini sana.

Falsafa yake ni mambo taratibu na kukuza, mashabiki wanataka haraka na makombe. Ameamua kunyoosha mikono na kumwaga mamilioni kwa timu nyingine ili kutimiza kinachotakiwa.

Wenger ni kamanda aliyenyoosha mikono kwa nia nzuri. Aliyekubali kushindwa ili ashinde na kuondoa presha.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic