July 10, 2017


Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, tayari ametua nchini juzi usiku akitokea kwao Cameroon alipokuwa ameenda kwa ajili ya mapumziko na leo hii anatarajia kuanza kazi ya kukisuka upya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Harakati zake hizo za kukisuka kikosi hicho zitaanzia katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam.

 Omog alisema kuwa anatarajia amerudi nchini kwa kazi moja tu ya kuhakikisha anakisuka upya kikosi hicho ili msimu ujao kiweze kufanya vizuri katika michuano ya ligi kuu na ile ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumzia usajili wa timu hiyo, alisema kuwa ni mzuri na wachezaji wote waliosajiliwa mpaka sasa anawajua, hivyo kazi kubwa atakayokuwa nayo ni kuwaunganisha ili waweze kucheza kitimu.
“Tayari nipo nchi tangu jana usiku (juzi) na kesho (leo) natarajia kuanza kazi yangu ya kukisuka upya kikosi changu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu.


“Imenibidi nirudi mapema kwa ajili ya kuanza mikakati yangu ya kuhakikisha msimu ujao tunakuwa na timu bora zaidi ukizingatia kuna wachezaji wengi wapya wamesajiliwa hivyo unatakiwa muda mrefu kuwaunganisha na wale waliokuwepo ili waweze kuendana na mifumo yangu,” alisema Omog.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV