July 5, 2017Na Saleh Ally
WASOMAJI wengi waliopiga simu za kutoa maoni kuhusiana na michuano ya Kombe la Mabara walitoa pongezi kwa gazeti la Championi kuifuatilia mwanzo mwisho.

Kwa upande wa runinga, wengi walipongeza StarTimes kwa kazi nzuri ya urushaji wa moja kwa moja michuano hiyo iliyofanyika nchini Russia na mwisho Ujerumani ikaibuka na ubingwa.

Wakati michuano hiyo inaanza, asilimia kubwa ya wachambuzi walitoa nafasi kwa Ureno na Chile kwamba zina nafasi kubwa sana ya kubeba ubingwa huo.

Ujerumani na Russia zilionekana zinafuatia na Cameroon, Australia na New Zealand kama kawaida hazikuwa na nafasi hata kidogo ya kupewa nafasi ya kugusa kombe hilo na ndiyo ilionekana ni hali halisi.

 Ureno ilipewa nafasi kwa kuwa inaongozwa na mchezaji nyota zaidi duniani, Cristiano Ronaldo lakini wako nyota kama Nani, Ricardo Quaresma na wengineo.

 Chile wao wana Alexis Sanchez, Arturo Vidal na wengine kibao. Nani angewazuia na wanajulikana kuwa wana uwezo mkubwa na msaada katika klabu zao.

 Ujerumani, ilionekana inawakosa nyota wengi kama Mesut Ozil, Thomas Muller na wengine ambao walitarajiwa kuonekana katika kikosi hicho lakini haikuwa hivyo.

Unaweza kujifunza mambo mengi sana kupitia Ujerumani kwamba ni watu wanaofanya vitu vyao vingi katika maisha kwa mpangilio sahihi na mwendo unaotakiwa bila ya kupoteza au kuvuruga kitu.

Ndani ya miaka mitatu, Ujerumani imetwaa mataji manne makubwa ambayo ni hili la Mabara, Kombe la Dunia, Kombe la Ulaya kwa Vijana chini ya Miaka 21 (U-21) na Kombe la Ulaya kwa Wanawake.

Programu ya utengenezaji timu ya taifa, utaona sasa wamechukua Kombe la Mabara kwa mara ya kwanza lakini wakiwa wameandika mambo mengi sana kama rekodi.

Kwanza wametengeneza kikosi kipya kabisa ambacho hakuna ubishi kinaweza kushiriki Kombe la Dunia. Lakini lazima watawaongeza wakongwe ambao walibeba Kombe la Dunia mwaka 2014 huko Brazil. Jiulize kikosi chao kitakuwaje?

 Wajerumani walianza kuwaandaa wachezaji walioitumikia timu ya Kombe la Mabara mara tu baada ya kwisha kwa Kombe la Dunia nchini Brazil. Walifanya hivyo kwa kuwa kila kitu kwao kinakwenda kwa hesabu na walijua wachezaji wengi kama Phillip Lahm, Bastian Schweinstaiger na wengine kadhaa watakuwa wamestaafu lakini Muller na baadhi yao hawatakuwa na kasi kubwa na kilichotakiwa ni kumtengeneza na kumfanya Lars Edi Stindl na wenzake wajiamini.

Bado Muller atakuwa na nafasi ya kuingia kama mkongwe kama ambavyo Mario Gotze amekuwa akitumika. Na huu umekuwa ni mfumo endelevu miaka nenda rudi.

Angalia Ureno au Chile ambao wamewachezesha wachezaji walewale waliotwaa ubingwa wa Euro na Copa Amerika kwa asilimia 80, maana yake hawakuwajenga wachezaji wengi zaidi kwa ajili ya Kombe la Dunia au michuano mikubwa ijayo.

Hali kadhalika, hali hiyo ilikuwa kwa Chile. Angalau Russia kidogo waliingiza vijana lakini nao walilaumiwa kuwatumia wachache sana, huenda kutokana na presha ya uenyeji, walitaka kushinda angalau Kombe la Mabara.

Wajerumani wamekuwa si waoga kwa kuwa mambo yao mengi yanakwenda kwa mpangilio sahihi sana.

Wamemaliza michuano hiyo wakiwa wamebeba ubingwa lakini wachezaji wake watatu Timo Werner, Leon Goretzka na Stindl wamekuwa wafungaji bora maana kila mmoja kafunga mabao matatu ila Werner kachukua kiatu kwa kuwa alikuwa na asisiti 2.

Mchezaji bora wa michuano ni Julien Draxler, aliyeshika nafasi ya pili ni Sanchez kutoka Chile na nafasi ya tatu imeenda kwa Goretzka naye ni Ujerumani.


 Timu yenye mchezo bora na wa kiungwana ni Ujerumani pia. Sasa wewe mwenyewe unaweza kuangalia na kujifunza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV