Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea malalamiko kutoka baadhi ya timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji vya soka zikidai fidia baada ya wachezaji wao kusajiliwa na klabu nyingine msimu wa 2017/18.
Jana Agosti 14, 2017 ilikuwa siku ya mwisho kwa timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji kuwasilisha malalamiko yao TFF kuhusu fidia za mafunzo; ada ya usajili; ada za maendeleo na kuvunjwa kwa mikataba kutoka katika timu walizochezea hadi msimu uliopita.
TFF imepokea malalamiko ya Kagera Sugar ya Kagera dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam kuhusu mchezaji Mbaraka Yussuf wakati Majimaji ya Songea pia imelalamika Azam kuhusu mchezaji Idd Kipangwile.
Alliance ya Mwanza imelalamikia Pamba pia ya Mwanza kuhusu mchezaji Juma Nyangi ambako madai hayo yamekwenda mbali zaidi yakisema kuwa mchezaji husika amebadili jina kwa lengo la kudanganya.
Kwa upande wake, African Lyon imeondokewa na wachezaji 19 na inadai fidia katika timu, wachezaji kwenye mabano za Majimaji (Saleh Malande); Lipuli (Hamad Manzi, Lambele Reuben na Mussa Nampoka); Young Africans (Rostand Youthe Jehu); Tusker FC (Abdul Hilal) na Ndanda kwa wachezaji Hamad Tajiri na Baraka Majogoo.
Madai mengine ni dhidi ya Coastal Union kwa wachezaji Baraka Jaffary, Omary Salum, Raizen Hafidh na Fred Lewis huku madai mengine ni kwa Kagera Sugar kwa wachezaji Omar Abdallah, Abdallah Mguhi na Vicent Ludovic na Alhaji Zege .
Madai mengine ni dhidi ya timu ya Kinondoni Municipality Council (KMC) ambayo imewasajili Halfan Twenye, Yussuf Abdul na Rehani Kibingu wakati Singida United inalalamikiwa kumsajili Miraji Adam ilihali Njombe Mji inadaiwa fidia kwa kumsajili mchezaji Salum Juma.
Malalamiko mengine ni ya Kisa Academy ya Kinondoni, Dar es Salaam dhidi ya timu za Mbeya City (Idd Seleman); Majimaji (Jafar Mohammed); Mbao (Ally Rashid); Stand United (Said Mbati) na Friends Rangers (Hassan Abubakar).
Madai mengine dhidi ya timu za Coastal Union (Abubakar Nyakarungi na Ahmed George); The Mighty Elephant (Maliki Hamad); Kagera Sugar (Hussein Idd) na Azam FC (Omary Maunda).
Kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kinatarajiwa kuketi Jumapili kupitisha usajili lakini kabla kitapitia malalamiko hayo na kuchukua uamuzi.
0 COMMENTS:
Post a Comment