September 8, 2017


 “NILIANZA kucheza soka la mtaani, lakini baadaye kuna kocha Mzungu alikuwa anainoa Ma­jimaji, anaitwa Sam­solov, aliniona na ku­taka kunipeleka Ulaya kuniendeleza kisoka, alipoenda kwa wazazi wangu baba akakataa, lakini yule Mzungu akawaambia Majimaji kwamba wanilee vizuri kwani ni hazina kubwa nitakuja kuwasaidia hapo baadaye,” anaan­za kusimulia nyota wa zamani wa Taifa Stars na Simba, Steven Ma­punda ‘Garincha’.


Garincha atakum­bukwa zaidi na Wa­nasimba kutokana na kukabidhiwa unahodha na kufanikisha kuwaon­dosha waliokuwa mab­ingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek, mwaka 2003.


Anasema katika mai­sha yake ya soka, ame­fanikiwa kucheza timu mbili tu za klabu zilizo­shiriki Ligi Kuu Bara. Timu hizo ni Simba na Majimaji, alianzia Majimaji kabla ya kuhamia Simba.


“Nimezaliwa mwaka 1975 katika Kijiji cha Luwanda kilichopo Wilaya ya Mbinga mkoani Songea, nimekulia na kusoma hukohuko.

“Baadaye nikiwa na wazazi wangu, tukahamia Songea Mjini ambapo mpaka sasa nipo hapo na familia yangu kwani nimejenga.

Baba kuzuia kuondoka na Mzungu

“Sasa baada ya yule Mzungu ombi lake kufeli kutokana na baba yangu kukataa mimi kuondoka naye, Majimaji kweli walinilea na baadaye nikaja kuwa mchezaji wao kuanzia mwaka 1997 mpaka 1999.


“Kabla sijajiunga na Majimaji, niliwahi kucheza Tigger ya Mbeya, ilikuwa ikishiriki ligi za madaraja ya chini. Nilipokuwa Maji­maji, niliisaidia kuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu wa mwaka 1998.


“Kikubwa ninachoweza kusema ni kwamba, ni­kiwa Majimaji, mafanikio makubwa niliyoyapata ni kuchukua ubingwa huo wa ligi, lakini pia kwa miaka yote tulikuwa tukicheza Kombe la Mu­ungano ambalo lilikuwa likihusi­sha timu sita, tatu za Tanzania Bara na tatu kutoka Zanzibar.


“Kwa tafsiri ya harakaharaka ni kwamba, kwa muda wote niliokaa Majimaji, hatukuwahi kutoka ndani ya tatu bora ndiyo maana tulikuwa tukishiriki mi­chuano hiyo ambayo huchukua timu tatu za juu kutoka ligi ya Bara na ile ya Zanzibar.


“Baada ya kucheza kwa kiwango kikubwa ndani ya Majimaji, mwishoni mwa mwaka 1999, nikafanikiwa kujiunga na Simba.

“Aliyefanikisha mpaka mimi kujiunga na Simba ni mfan­yabiashara, Moham­med Dewji ‘Mo’ kwani alikuwa anavutiwa sana na kiwango changu.

“Kabla ya hapo, Yanga waliwahi kunifuata kama mara mbili hivi, lakini walishindwa kun­iondoa kutokana na kukutana na vikwazo mbalimbali kwa watu ambao hawakuwa tayari kuniona naondoka Majimaji.

“Simba nilicheza mpaka mwaka 2006 nilipoamua kurudi ny­umbani Majimaji.

“Nikiwa Simba, tukio ambalo nalikum­buka mpaka leo ni kitendo cha sisi ku­waondoa Zamalek ya Misri wal­iokuwa mab­ingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tuli­waondoa mwaka 2003 na kut­inga robo fainali ya michua­no hiyo bila ya wengi kutarajia. Wakati huo mimi nilikuwa nahodha.

Anatu­kumbusha kidogo ilivy­okuwa

“Kwanza kabisa nikuta­jie baadhi ya wachezaji wal­iokuwa kwenye kikosi cha kwanza. Aliku­wepo Selemani Matola, Boniphace Pawasa, Juma Kaseja na Ramad­han Waso.

“Nakumbuka maandalizi ya mechi hiyo hayakuwa ya kutisha sana, la­kini naweza kusema jukumu nililopewa kwa kiasi kikubwa lilichangia tukasonga mbele.

“Ilikuwa hivi, baada ya kwenda Zambia kucheza dhidi ya Nkana, kuna wache­zaji wetu watano wa kikosi cha kwanza walikuwa wamefun­giwa wasicheze mechi ya marudiano, hivyo Kocha Aggrey Siang’a akanipa jukumu la kuwaongoza wen­zangu. Yaani nikapewa unahodha.

“Kwanza nilimwam­bia kocha kuwa mimi siwezi majukumu hayo, alipoona naen­delea kumkatalia ombi lake, akaamua kuwaita wazee waweze ku­niweka chini ili niku­bali, mwisho wa siku nikakubali.

“Mechi ya marudi­ano, tuliwafunga 3-0, ilipigwa Uwanja wa Jamhuri, Mo­rogoro. Ikafuata mechi dhidi ya BDF XI ya Bot­swana. Hapa nyumbani tukawafunga bao 1-0, bao hilo nilili­funga mimi.

“Kutokana na ush­indi huo kuonekana ni mdogo, Watanzania wakaona ndiyo mwisho wa safari yetu, hakuna aliyetupa nafasi ya kusonga mbele.

“Cha kushangaza ni kwamba, tulipoenda kwao tukawafunga 3-1, tukasonga mbele. Tukacheza na San­tos ya Afrika Kusini, mechi zote zikawa 0-0, tukasonga mbele kwa penalti 9-8. Ilipomal­izika mechi hiyo, mechi iliyofuata ndiyo ilikuwa dhidi ya Zamalek.

“Kabla ya mechi hiyo nakumbuka alikuja Waziri Mkuu Frederick Sumaye, tukafanya kikao Uwanja wa Taifa ambao sasa unaitwa Uwanja wa Uhuru.

“Majadiliano yakaan­za kufanyika kwamba tufanye nini ili tuweze kuwaondosha Zamalek kwani mara kadhaa timu za Waarabu zime­kuwa zikizisumbua sana timu za Tanzania na kuzitoa kila zinapoku­tana.

“Wakati majadiliano yakiendelea, wazee wa klabu wakanisimamisha ili niweze kuzungumza kwa niaba ya wen­zangu.

“Binafsi nakumbuka miongoni mwa maneno niliyomwambia waziri ni kwamba tunatakiwa ku­fanya mambo ambayo yatatufanya tusonge mbele bila ya wasiwasi, ikitokea tumeshindwa labda bahati mbaya.

“Nilimwambia kwanza sisi ni masi­kini na wapinzani wetu huwa wanatumia sana udhaifu huo kutufunga kila tunapokutana nao.

“Kutokana na umasi­kini wetu, tunapoenda kwao hutugharamia kwa kila kitu, katika kufanya hivyo, kuna mambo huyafanya ya kiujanjaujanja, wanatu­funga kirahisi.

“Sasa nikamwambia haya mambo yote sijui ya kutafuta hoteli ya ku­fikia tufanye wenyewe, nikasema kama hatuna uwezo huo basi tupo radhi kufikia hata uba­lozini, tutalala kwenye magodoro. Tukamaliza kikao kwa makubaliano kwamba mambo yote tutafanya wenyewe.

Wiki ijayo Mapunda atazungumzia kuhusu zawadi aliyowahi kupewa na Mo, anayo mpaka leo, pia atafunguka kuhusu mamilioni ya Sokabet yatakavyoinufaisha Majimaji.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic