September 4, 2017




Na Saleh Ally, Manchester
BINAFSI nimeamua kuchagua kujifunza kila kukicha hadi mwisho wa maisha yangu yote. Huu ni uamuzi binafsi unaohusisha imani yangu kutokana na mambo ambayo nimepitia kwa takribani miaka 20 ya kushiriki katika michezo.

Kujifunza ni jambo jema zaidi kwa kuwa kila unapopokea mafunzo fulani basi unagundua ulichokuwa unakijua awali kimepungukiwa jambo fulani ambalo hukulitegemea.

Kabla ya kujifunza jambo, wanadamu tuna tabia ya kuamini tuko vizuri na tunajua vitu vingi. Lakini unapotoa nafasi ya kujifunza jambo jipya basi unagundua kuwa haukuwa unajua kama ulivyokuwa unafikiri.

Elimu ni jambo jema na wakati mwingine vizuri kuifuata kokote inapopatikana kuliko kusubiri ikukute ulipo utafikiri yenyewe ndiyo ina shida na wewe.

Niko jijini Manchester ambako nimeanza ziara yangu ya mafunzo, Mungu akijaalia leo nitaondoka kwenda jijini London kumalizia ziara hii ya mafunzo.

Nikiwa Manchester siku ya nne leo, nimejifunza mambo mengi sana lakini kubwa ni namna ambavyo wenzetu wanautumia mpira kama biashara kubwa kabisa kuliko sisi tunavyoamini ni ushabiki kuonyesha machungu kuwa wewe ni shabiki wa timu fulani.
Wengi tunaamini kuonyesha unaipenda timu fulani inatosha sana na wakati mwingine ndiyo jambo la mwisho kabisa. 
Lakini wako ambao hasa kwa upande wa viongozi wanaamini kuwa timu moja kuifunga nyingine ndiyo kazi pekee ambayo inatakiwa kufanywa na kiongozi.

Yote haya ni sawa lakini kwa kiwango cha chini kabisa kwa kuwa ni sehemu ndogo sana kwa viongozi na wengine yaani mashabiki kwamba wanatakiwa kwenda zaidi ya hapo.

Unapofika katika Jiji la Manchester, asilimia 60 ya watalii wa jiji hili wanaonekana wako hapa kuutembelea Uwanja wa Old Trafford na kiasi Uwanja wa Etihad ambao unamilikiwa na Manchester City.

Old Trafford mali ya Manchester United ni kivutio cha utalii kama ambavyo watalii hutua nyumbani Tanzania kwa ajili ya kwenda kuangalia wanyama mbugani au kutembelea katika fukwe zenye mvuto kule Zanzibar.

Wenzetu hawana wanyama kama ilivyo sisi ambao watu wangefika kuwaangalia. Hata fukwe zao si zenye mvuto kama ilivyo za kwetu lakini wanaingiza fedha nyingi za utalii kupitia mpira, jambo ambalo hawajapewa na Mungu kama ilivyo kwetu lakini wametumia akili zao za ziada.

Akili za ziada kwa kuwa wameangalia kibiashara zaidi jambo ambalo linataka ubunifu na kujituma bila ya kuchoka. Lakini sisi bado tumebaki kwenye kuamini soka ni burudani na mmoja kumfunga mwingine basi inatosha na kazi inakuwa imeisha, hili si jambo jema hata kidogo.

Mmoja wa dereva teksi wa hapa Manchester ameniambia wanaingiza fedha nyingi kupitia watalii wanaokuja kuutembelea Uwanja wa Old Trafford pia Etihad ingawa ni kwa kiwango kidogo sana.

Ameniambia wanaona ushabiki wao una faida na wako tayari kusaidia kwa mawazo ili kuhakikisha timu hiyo inafanikiwa kufanya vema badala ya kufa.
Yeye ni shabiki mkubwa wa Man United na haipendi kabisa Manchester City. Lakini angependa kuona Man City inaendelea kuwepo ili kuongeza ushindani unaolitangaza jiji hili ili wapate mambo mawili.

Kitu cha kwanza anachotaka ni furaha ya moyo ambayo hata mashabiki wa kwetu wanaipata. Lakini pili ni fedha, anaingiza kutokana na timu hizo kuwa na mashabiki wengi wakiwemo wale wanaotokea nje ya England ambao wanaonekana ni wengi zaidi.

Shabiki wa Tanzania unafaidika na nini na timu yako? Furaha pekee inaposhinda na maudhi inapofungwa? Kingine? Umewahi kujiuliza pia unaisaidiaje iendelee kuwepo pamoja na mpinzani?

Lazima tujifunze kwamba soka ni fedha nyingi sana na klabu sasa zifanye kazi kwa kushirikiana na wataalamu wa biashara wenye mlengo wa soka wanaoweza kujua utajiri ulipojificha kuliko kuendelea kufanya kama tulivyo sasa. Tunacheza ngoma, wimbo ni kilio cha njaa lakini ukumbi wa shoo yenyewe uko juu ya mgodi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic