September 4, 2017



Huku Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, akijipanga kumtumia mshambuliaji wake mpya raia wa Ghana, Nicholas Gyan dhidi ya Azam FC, mchezaji huyo juzi Jumamosi alishindwa kufanya mazoezi na timu hiyo kwa sababu ya begi.

Hiyo lilikuwa ni pigo na balaa kwa Simba pamoja na Omog ambaye akili yake yote ni kushinda mchezo wake ujao dhidi ya Azam na angependa kuwaweka fiti wachezaji wake kiakili na kinguvu kuelekea mchezo huo.

Gyan ambaye amesajiliwa na Simba hivi karibuni akitokea Ghana, hakuweza kufanya mazoezi na timu hiyo baada ya kukosa vifaa vya mazoezi kutokana na kupotelewa na begi lake liliokuwa na vifaa hivyo pamoja na nguo zake nyingine wakati alipokuwa safarini akitokea kwao nchini Ghana.

Kutokana na hali hiyo alijikuta akiwa mtazamaji wakati wachezaji wenzake wa Simba walipokuwa wakijifua kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao ya ligi kuu dhidi ya Azam ambayo awali ilikuwa imepangwa kufanyika Jumatano hii lakini sasa imesogezwa mbele mpaka Jumamosi, Septemba 9, mwaka huu.
Gyan amekumbana na balaa hilo Jumamosi alfajiri baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA) akitokea Ghana ambapo hakuweza kuliona begi lake hilo.

Kitendo hicho kinadaiwa kumvuruga vilivyo, jambo ambalo pia lilimsikitisha Omog ambaye alikuwa akimsubiri kwa hamu kubwa mchezaji huyo katika mazoezi hayo.

Omog alisema kuwa uongozi wa timu hiyo unalishughulikia suala hilo ili Gyan aweze kupata begi lake hilo lakini pia kwa upande wake yeye anajipanga kuhakikisha anamweka sawa kiakili ili aweze kumtumia kwenye mechi hiyo dhidi ya Azam.

“Taarifa za kupotelewa begi lake nimezisikia lakini najua uongozi utakuwa unalishughulikia ila binafsi nimefurahia ujio wake na sasa najipanga kuhakikisha anakuwa sawa kwa ajili ya mechi yetu dhidi ya Azam.


“Ninajitahidi kumweka sawa kiakili ili aweze kulisahau suala hilo lililomtokea kabla ya kukabiliana na Azam, kwani tunataka kupata ushindi dhidi yao ili tuendelee kuwa juu katika msimamo wa ligi,” alisema Omog.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic