Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa muda kwamba hadi Septemba 22, klabu zote 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na za zile 24 Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ziwe zimekamilisha taratibu za kupata Leseni za Klabu.
Kwa mujibu wa Kamati ya Leseni za Klabu, ni timu tano za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya 16 hazikuchukua hata fomu za maombi ya Leseni za klabu wakati Klabu 11 zimebainika kuwa na upungufu mkubwa katika kukamilisha vigezo.
Kamati ya Leseni za Klabu imekutana zaidi ya mara tatu katika vikao na kujiridhisha kwamba kwa ujumla vigezo vifuatavyo havijakamilika kwa asilimia 100 katika klabu nyingi kama zifuatavyo.
1. Klabu zote hazina programu ya kuendeleza mpira kwa vijana.
2. Taarifa za klabu haielezi kuhusu miundombinu ya kuhudumia walemavu wakati wa mchezo.
3. Klabu hazijaonesha uwanja wa mazoezi.
4. Hazijaambatanisha mikataba ya watendaji kama vile Katibu Mkuu; Ofisa Usalama wa timu, Mhasibu au mkurugenzi wa fedha, na daktari n.k.
5. Taarifa hazina maelezo ya kocha wa timu za vijana.
6. Klabu hazijajaza fomu za kuomba Leseni ya klabu.
7. Hazijambatanisha katiba ya klabu.
8. Klabu hazijaambatanisha ripoti ya fedha ya mwaka.
9. Klabu hazijajaza fomu ya kuthibitisha kushiriki mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom.
Kwa taarifa hii kwa umma, Kamati ya Leseni ya Klabu inazitaka klabu kukamilisha vigezo hivyo kabla ya Septemba 22, mwaka huu. Vinginevyo, klabu inaweza kuondolewa kwenye mashindano.
0 COMMENTS:
Post a Comment