NA SALEH ALLY
UNAPOKUWA unakosoa bila ya woga, basi inakuwa vizuri sana ukawa pia unasifia bila ya kuhofia lawama kutoka upande wowote ule.
Mashabiki wa Simba wamekuwa ni kati ya wale ambao wana wakati mgumu sana hasa baada ya mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara kwenda mbele.
Ugumu wao umekuwa ni kutokana na hali ilivyo. Tofauti kabisa na namna ambavyo waliitarajia wao wakati ligi inaanza.
Kutokana na usajili wa “kukata na mundu” waliokuwa wamefanya Simba, mashabiki wengi waliamini mambo yatakuwa ni “ganda la ndizi”, yaani utelezi kwa kila timu watakayokutana nayo.
Wako wale ambao si wavumilivu na wavivu kutuliza mambo na kutafakari, walianza kulaumu kwamba waliaminishwa na vyombo vya habari timu yao ni nzuri. Lakini ukweli uko hivi, kweli Simba ni nzuri na wala si uongozi.
Ugumu wa ligi hiyo umeifanya kila timu iwe katika wakati mgumu ikiwemo Simba ambayo ilionekana haitakuwa na shida wala wa kuizuia.
Nafikiri badala ya mashabiki kuendelea kuzilaumu timu zao kama ambavyo wanafanya wengine mfano wale wa Yanga ambao lawama nyingi humuangushia Kocha George Lwandamina, basi wajiulize na mazingira yalivyo.
Achana na kuangalia wachezaji majeruhi pekee. Badala yake mashabiki hao wanaweza pia kujifunza jambo nje ya timu zao. Angalia Ligi Kuu Bara ilivyo kwa kuwa kuna bahati kupitia runinga ya Azam FC ambayo huonyesha moja kwa moja.
Ukweli kwamba kwa sasa Ligi Kuu Bara imekuwa ngumu ukilinganisha na misimu mitano iliyopita lakini imekuwa ngumu zaidi ukilinganisha na misimu miwili au mmoja uliopita.
Angalau unaweza kusema suala la haki kutoka kwa waamuzi, limechukua nafasi kubwa na kweli, hakuna tena masuala ya uongozi wa TFF kuingilia na kuingiza masuala ya ushabiki.
Safari hii viongozi wa TFF wanaonekana wamekuwa makini, wamejiondoa katika eneo hilo na kuacha taaluma ifanye kazi yake kama inavyotakiwa na tunakubaliana waamuzi wengi wanajitahidi.
Makosa ya kibinadamu hayatakosekana na hilo liko wazi lakini makosa ya makusudi kwa baadhi ya waamuzi ambao si waaminifu pia yatakosekana.
Pamoja na hivyo tukubaliane kwamba kama kuna tatizo, kawaida linaondolewa kwa kuanza kupunguzwa na baadaye kulifutilia mbali kabisa.
Tatizo la waamuzi kuchukua hongo lilikuwa kubwa na kwa kuwa lilihusisha baadhi ya viongozi wa TFF wenye mapenzi au ushabiki au kushiriki katika kujipatia kitu kidogo, ikawa shida kubwa.
Tumeona waamuzi wakiboronga na wasichukuliwe hatua kwa kuwa waliiadhibu timu ambayo haipendi bosi, au walifanya hivyo makusudi kwa maagizo ya bosi na hili liko katika ushabiki wa Simba na Yanga na tunalijua ingawa wengi wana hofu ya kulisema hadharani.
TFF ya sasa inaonekana kuwatisha waamuzi wanaovuruga mambo kwa kuwa inapofikia wamevuruga, basi kamati zake hukaa mapema na kuchukua hatua na adhabu zimeanza kuonekana kuwa ni kali na wale wanaovuruga mambo wanaonekana wanaanza kuogopa.
Hatuwezi kusema waamuzi wote ni watu wa kuboronga tu. Wako wanaojitahidi na tunaona lakini wanaangushwa na wachache wasio waaminifu.
Tukubaliane, sehemu ya waamuzi ni muhimu sana katika maendeleo na mabadiliko ya soka. Wakiendelea kuwa makini namna hii na ikiwezekana ugumu huu uendelee kuongezeka, basi tujue tunakaribia kuingia katika kundi la ligi ngumu na bora.
Pia tukumbuke, ligi inapokuwa ngumu na bora, basi inazalisha wachezaji wengi na timu zilizo bora na itasaidia wachezaji wengi kupata soko hata nje ya Tanzania na mwisho tutajenga timu bora ya taifa.
0 COMMENTS:
Post a Comment