December 22, 2017



NA SALEH ALLY
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) ndiye msimamizi wa masuala ya soka nchini na sasa kuna uongozi mpya chini ya Wallace Karia ambao unatupa matumaini makubwa.

Nasema uongozi huu unatupa matumaini makubwa kwa kuwa Watanzania tumepitia katika mengi yanayohusiana na maumivu wakati wa uongozi wa aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Unajua makosa na upungufu wa uongozi uliopita na nilizungumza mara nyingi, nisingependa iwe leo. Lakini matumaini yanakuja kwa kuwa TFF iliyoingia inaonekana ina watu waliolenga kurekebisha mambo.


Subira ni jambo ambalo nimelitanguliza kwa kuwa nami ni kati ya wale wenye matumaini makubwa nikiamini makosa yaliyokuwa yakifanyika wakati wa Malinzi, sasa ni wakati mwafaka wa kuyarekebisha na hakutakuwa na vituko vingi badala yake matukio yaliyolenga mabadiliko.

Juzi kimetokea kituko baada ya mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Ajabalo dhidi ya Prisons ya Mbeya kushindwa kufanyika kutokana na baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wamesajiliwa na Abajalo kuwa hawajapitishwa na kamati husika ya TFF.


Hawakuwa wamepitishwa kwa kuwa kulikuwa na tatizo katika mfumo wa usajili kupitia mtandao na TFF wenyewe walitangaza kuongeza muda baada ya mfumo huo kupata shida.


Lakini cha ajabu kabisa, wakati TFF wakijua kwamba kuna tatizo, hawakuwa wametangaza kuahirishwa kwa mechi zilizokuwa zinafuatia za Kombe la Shirikisho ikiwemo hiyo kati ya Abajalo dhidi ya Prisons.


Wakati timu hizo zinakwenda uwanjani, tayari mfumo ulikuwa umetengemaa baada ya TFF kutangaza kwamba hali imekuwa hivyo. Lakini kwa kuwa kawaida ni lazima kamati ikae, wale wachezaji wa Ajabalo FC wakawa hawajapitishwa.


Abajalo FC kwa kuwa walifuata taratibu na halikuwa kosa lao, wakataka kuwachezesha wachezaji hao na huenda waliamini wangekuwa ni msaada kwao kwa kuwa walikuwa wanakutana na timu ngumu ya Ligi Kuu Bara, Prisons.

Pia inawezekana kabisa, Abajalo waliamua kuingia gharama kubwa wakiwa wamepania pia kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Shirikisho ya Azam Sports kwa kuimaliza Prisons, hivyo ilikuwa ni lazima wawatumie siku hiyo lakini haikuwezekana.

Uongozi wa Prisons wao walisimamia kanuni na kusisitiza wachezaji wanaocheza ni lazima wawe wamepitishwa na kamati na hiyo ni kwa mujibu wa kanuni.
Abajalo nao walisisitiza kwamba walifuata kila hatua na halikuwa kosa lao badala yake ni la TFF. Awali kulikuwa na taarifa kwamba TFF wangetoa vibali vya muda.


Lakini unajiuliza, vipi TFF imeshindwa kuitumia kamati yake ikae kwa dharura? Kama ilishindikana kwa nini TFF ilishindwa kuzisogeza mechi za Kombe la Shirikisho hasa za juzi ikiwezekana na siku mbili mbele ili mambo yakae sawa?
Nashangazwa na kuona mambo yameanza kwenda hovyo kwa kuwa kama TFF inashindwa kulifanyia kazi jambo kama hilo, inaonekana kuna tatizo katika utendaji wake kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi.

Kama itakuwa imekosea Bodi ya Ligi, TFF inapaswa kusimamia sahihi lakini TFF pia inapaswa kusaidia na bodi hiyo kuweka mambo sahihi.

Pia TFF inapaswa kuwajali wanachama wake ambao ni klabu, kama mechi imeahirishwa lazima wajue Prisons wametumia gharama kufika Dar es Salaam na wangeweza kuambiwa mapema.

Kwani TFF hawajui kama kuna kanuni? Hawakujua bila hivyo wachezaji wa Abajalo hawatacheza? Kilichotokea inawezekana Rais wa TFF, Wallace Karia hahusiki kabisa lakini kwa kuwa ndiye kiongozi mkuu na anaonekana kushindwa kusimamia sahihi, basi hili litamhusu na hata kama tumemkaribisha kwa lengo la kusaidia kuleta marekebisho na mabadiliko, basi tutaanza kumsema bila ya kuchoka hadi atakapofanya mambo yaende sahihi.



1 COMMENTS:

  1. Tatizo moja tulilo nalo watanzania ni kulazimisha uelewa wamambo na maoni yetu ndiyo yawe ukweli. Salehe, umesema tatizo ni mfumo wa usajili wa TFF kupata hitilafu kwa sababu ya mtandao, hakiki hilo si kosa la TFF. Na suala hilo halingeweza hata kidogo kuahirisha mechi kwa sababu tu eti timu zimesajili wachezaji wapya na ili wawatumie wanapaswa kupewa vibali. Hakuna mantiki hata, kidogo. Kama ili wachezaji wacheze ni laima wawe wamepitishwa na TFF na kupewa vibali, wachezaji wa Abajalo waliosajiliwa katika dirisha dogo wasingecheza (na hawapaswi kucheza) kama hawakuwa na vibali. Na wala hiyo haikuwa lazima eti ni sharti wawatumie. Abajaloilikuwa na wachezaji waliokuwa na nao tangu mwanzo kabla ya usajili huu mdogo, hivyo, hata kama wale waliongezwa hawakupatiwa vibali bado Abajalo wangechezesha wale waliokuwa nao. Kma hitilafu katika mfumo wa usajili isingelikuwepo taratibu zote zingelikuwa zimekamilika. Chukulia mfano wa timu za ligi kuu, je zingeshindwa kuingia uwanjani kucheza kwa sababu tu wanataka wachezaji wao waliosajiliwa wacheze wakati hawana vinali? Hakuna kosa kwa TFF, hakuna kosa kwa Prisons kutaka kanuni zifuatwe; kosa liko kwa Abajalo ambao walitaka kukiuka kanuni kuwachezesha wachezaji ambao hawajaidhinishwa, ambao hawana vibali.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic