December 13, 2017



Na Saleh Ally
NILIANZA kuona kitu cha ajabu kabisa pale baadhi ya mashabiki walipoishambulia Tanzania Bara kwa matusi makali bila ya kujali umri wao au kutukana kwa uwazi kuwa si jambo sahihi hata kidogo.

Vijana hao kutokea Zanzibar wanaonekana wakiwa na furaha kuu baada ya Zanzibar kuifunga Tanzania Bara kwa mabao 2-1 katika michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya.
Ilikuwa mechi bora kabisa kwa Zanzibar ambayo ilitoka nyuma kwa bao moja na mwisho kufanikiwa kushinda kwa mabao 2-1 tena wakionyesha soka safi bila ya mjadala.

Ushindi wa Zanzibar ulikuwa mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii na watu wengi waliusifia sana wakionyesha kufurahishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na namna kikosi hicho cha Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilivyofanya kazi yake vizuri.
Mjadala huo ulikuwa mzuri na wengi wakiwalaumu wachezaji na makocha wa Kilimanjaro Stars kushindwa kufanya lolote na hasa Kocha Mkuu Ammy Ninje. Lakini ajabu kabisa, siku iliyofuata, video ya vijana hao ikaanza kusambaa mitandaoni wakimwaga matusi bila ya woga kuitukana Tanzania Bara, iwe timu, wachezaji, makocha au ikiwezekana Tanzania Bara yenyewe.

Vijana wale ni wadogo, lakini si wale wasioweza kutambua ubaya wa maneno machafu au wale ambao hawana taarifa kuhusiana na makosa ya kimtandao. Hakika lilikuwa ni jambo la kushangaza sana na mbaya zaidi, video hiyo ikaendelea kusambaa kwa kasi kubwa.

Wakati nikiwa katika hali ya kushangaa kabisa kuhusiana na hilo, nikaanza kuona video safari hii ikiwa ni ya wachezaji wa Zanzibar Heroes wakiwa nyumbani nao wanatukana matusi makali yasiyokuwa na tofauti na yale waliyoporomosha wale mashabiki!
Walikuwa wachezaji kama watano hadi sita, lakini ajabu kabisa ni kuwaona wachezaji wawili, Mudathiri Yahaya wa Singida United na Mohammed Issa ’Banka’ wa Mtibwa Sugar, hawa wote wanacheza soka Tanzania Bara.

Wakati wengine walikuwa wakiporomosha matusi akiwemo Banka, aliyekuwa akiwarekodi wenzake huku akiwahimiza kama wafanye jambo fulani, na walichokuwa wakifanya ni kutukana.

Hapo nilikuwa najiuliza, inakuwaje sasa kama ni Mudathiri huyu na Banka huyu wanaocheza Tanzania Bara na matusi wanayotoa hata kama ni chuki, inatokana na nini? Kama kweli tunawategemea kuwa wachezaji wa kulipwa, vipi wanaweza kujirekodi wakiachia matusi makali tena mtandaoni na wakaachia yasambae.

Achana na suala la kuwa wachezaji wanaofuata weledi, jiulize inakuwaje wao hawajui ni kosa kubwa kimtandao kutukana au lugha kali kama hizo tena ajabu kwa watu maarufu au wanaoheshimika kama wao?

Lakini tokea wametukana matusi hayo, hadi leo sijasikia kama kuna hatua za kinidhamu au kisheria zimechukuliwa.

Kwangu kwa kila aliyetukana namchukulia kama mtu anayehatarisha muungano wa Tanzania. Maana hii inaweza kutengeneza chuki na wanapaswa kuchukuliwa hatua ili hili liwe mfano.
Ukimya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) katika suala hili, unaonyesha kuna tatizo kubwa na wanakaribisha wengine kupitia soka kutengeneza chuki badala ya njia sahihi za muunganiko.

Vipi hadi leo TFF au ZFA hawajaonyesha kukerwa na jambo hilo baya kabisa katika mpira? Wakati kila upande hasa siasa na kadhalika wakipambana kuupigania muungano, kweli soka iwe chanzo cha kuuyumbisha na viongozi wake wanakaa kimya wakiona sawa?
Labda kwa yeyote kutoka Bara au hata Zanzibar anaona ni sahihi hicho kilichofanyika na kinapaswa kutetewa kwa kivuli cha Uzanzibari? Tena kimefanywa na wachezaji wanaojulikana na walio katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars? Haya ni maajabu ya karne na picha bora ya uzembe wa maisha yetu.

Wale vijana waliotukana matusi makubwa, nao wako huru, wako salama, hakuna anayewauliza na tunasema nchi yetu inapaswa kuwa na nidhamu kwa kuwa hakuna aliyelaani kwa maana ya vyombo husika wakiwemo wanaosimamia mitandao kama TCAA.

 Muungano unahitaji heshima kubwa, hata kama wale vijana au watoto wamekuta mambo yanakwenda basi wanaona kila kitu rahisi au wanataka kuyapeleka mambo kisela wakiona ni sawa na mambo ya mtaani tu.

Mimi nasisitiza, kuanzia wale vijana hadi wachezaji wachukuliwe hatua za kinidhamu kuhakikisha umakini na uhakika wa mambo kuepusha upuuzi uliojitokeza kuendelea kila mara.


Bara kufungwa na Zanzibar, kama imetokea ni suala la furaha upande mmoja na kujiuliza upande mwingine. Lakini si kutukanana kwa kisingizio cha furaha. Wakiadhibiwa hao, wengine watakuwa makini.

8 COMMENTS:

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  2. Na kubaliana na wewe mwandishi kwamba nidhamu na heshima ni kitu cha bure kwa mkubwa au mdogo sio vyema kuliachia suala hilo kupita bila ya kukemewa lakini pia na wewe umekwenda mbali sna suala michezo na kuvunjika kwa muungano ni wapi na wapi inabidi utafakari vizuri kwanza kabla ya kuandika kila la kheri na kazi njema.

    ReplyDelete
  3. NO COMMENT:
    Sijaiona hiyo clip kwahyo hata kuitolea neno nashindwa. Ila kama alivyosema hapo jamaa..tusiende beyond of what happened...twende kutokana na mipaka ya kile kilichotokea.

    Thanks

    ReplyDelete
  4. NO COMMENT:
    Sijaiona hiyo clip kwahyo hata kuitolea neno nashindwa. Ila kama alivyosema hapo jamaa..tusiende beyond of what happened...twende kutokana na mipaka ya kile kilichotokea.

    Thanks

    ReplyDelete
  5. Kwanini wasirudishiwe nchi yao? Liko jambo kubwa linaonekana kujificha ama kufichwa juu ya muungano wetu. Na kadri wanavyobanwa watu kuujadili ndivyo nafasi za watu kutema nyongo zao zinavyotumika popote wapatapo nafasi.
    Nidhamu na adabu huleta upendo lakini pia kutotaka kusikiliza sauti nyingine nako huleta majanga.

    ReplyDelete
  6. Daima ukikaa na mzanzibari au mpemba yeyote mazungumzo yao ni ya kibaguzi hapendi kabisa muungano ndo maana wanafanya hayo makusudi, kinadharia unawasaidia sana kuliko hata wa bara. Wataendelea kututukana

    ReplyDelete
  7. Sidhani kama michezo ndiyo njia ya kufikiria juu ya Muungano. Hiyo ni mihemko ya kimichezo na tunao wachezaji wengi wa Visiwani wakicheza kwa miaka mingi bila kuonekana tofauti kwenye usajiri wao. Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania Bara kufungwa na Zanzibar Heroes. Tukubaliane maandalizi ya Tanzania Bara hayakuwa makini. Huwezi kukusanya watu wa timu zenye falsafa mbalimbali kwa siku tatu, kisha utegemee kupata miujiza, jamani mpira si ndoo ya maji unateka bombani au kisimani kisha ukaenda kutumia nyumbani. Tuache lawama ila tujifunze kufanya maandalizi makini na kuwachukua watu wenye utalaamu kwenye mashindano? Mbona bingwa mtetezi Uganda kafungwa, Rwanda na mwenyeji Kenya kafungwa tunasemaje? Muungano unaingiaje, hebu tuache siasa na michezo.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic