Na Saleh Ally
KIKOSI cha Mbao FC, huenda kimewashangaza wengi kutokana na hatua kubwa kinachozipiga ikiwa ni siku chache baada ya kubomolewa na klabu kubwa za soka nchini.
Baada ya msimu wa 2016-17 kwisha, Mbao FC ilibomolewa baada ya wachezaji wake kwenda katika klabu kubwa za Yanga, Simba na Azam FC kwa ajili ya msimu wa 2017-18.
Kuondoka kwa wachezaji hao kulizua hisia za hofu kwamba huenda mwisho wa Mbao FC kufanya vema na kuwa tishio kwa vigogo ulikuwa ndiyo kuwadia.
Wengi waliona Mbao FC walikuwa wamekosea na huenda hata taarifa kuwa kocha wake, Etienne Ndayiragije kuwa alikuwa anatarajia kuondoka zilifanana sana na zile hisia za mashabiki kwamba huenda kocha huyo hakufurahia kuuzwa kwa nyota wake mfululizo.
Lakini baadaye kocha huyo raia wa Burundi aliendelea kubaki katika kikosi cha Mbao FC hadi sasa. Lakini kilichovutia zaidi ni namna alivyoweza kuijenga upya timu yake ikiwa bila ya wachezaji waliotegemewa msimu mmoja uliopita.
Utakuwa unakumbuka, kwamba kikosi hicho, msimu uliopita, kiliwavua Yanga ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports ikiwa ni pamoja na kuwaangusha kwa kipigo.
Lakini walipotinga fainali ya Kombe la Shirikisho ya Simba, pale Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kulichimbika kwelikweli na Simba waliuchukua ubingwa ule wakilala na viatu.
Msimu huu, Simba wamekutana na Mbao FC katika Ligi Kuu Bara, mechi hiyo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba iliisha kwa sare ya mabao 2-2, Mbao FC wakisawazisha mara zote.
Mechi nyingine na kigogo, ilikuwa dhidi ya Yanga juzi hapohapo CCM Kirumba, Yanga wamekubali kipigo cha mabao 2-0, hiki kikiwa cha pili mfululizo.
Wakati Mbao FC wanakutana na Yanga, kuna kitu unaweza kujifunza. Kwamba wanacheza kwa kujiamini, wanaonyesha soka safi lakini wanafunga mabao mazuri kabisa, kama ambayo walifunga dhidi ya Simba.
Mechi mbili dhidi ya Yanga na Simba, Mbao FC wamefunga mabao manne na wamefungwa mawili tu. Hii si timu ya kubeza na Ndayiragije, si mtu wa kumbeza tu.
Tokea mwanzo, nimezungumzia timu na baadaye nimegusa kuhusiana na wachezaji wanavyokuwa wanacheza wakijiamini na zaidi ningependa kumzungumzia mshambuliaji wa Mbao FC, Habibu Haji Kiyombo.
Kiyombo amefunga mabao matatu ya Mbao FC dhidi ya Yanga na Simba. Alifunga moja mechi ya 2-2 dhidi ya Simba lakini akarudia na kufunga mawili Yanga ilipolala 2-0.
Wakati Kiyombo anafunga mabao hayo, utaona huwezi kuona hata mshambuliaji mmoja wa Simba au Yanga mwenye mawili, au huwezi kuona washambuliaji wa kimataifa wa timu hizo kuwa walifanya vema dhidi ya Mbao FC.
Hiyo haitoshi, Kiyombo amefunga mabao matatu dhidi ya Yanga na Simba katika mechi hizo mbili. Lakini mabao yake mawili yanafanana kabisa na unaweza yote mawili ukayaingiza kwenye shindano la bao bora Ligi Kuu Bara.
Dhidi ya Simba, Kiyombo alimtoka beki mmoja, akiwa umbali wa takribani mita 25 hadi 28, akaachia mkwaju mkali uliomshinda Aishi Manula na kuandika bao la kwanza la Mbao FC.
Mechi dhidi ya Yanga, Kiyombo alirudia, safari hii akiwatoka mabeki wawili wa Yanga na kuachia mkwaju wa chinichini uliojaa moja kwa moja wavuni na kuandika bao la kwanza la Mbao FC dhidi ya Yanga kabla ya kuongeza la pili.
Unaweza kujiuliza, kijana huyu anapata wapi hali ya kujiamini na kufunga mabao matatu dhidi ya Yanga na Simba lakini mabao bora kabisa ambayo wakati mwingine ni vigumu kuona washambulizi wa kimataifa wanaocheza hapa nyumbani wakifunga mabao kama hayo!
Alijiamini nini au ana nini ambacho huenda hatujakiona na huenda ni nafasi nyingine ya kuanza kukitambua na kukifanyia kazi?
Tena kwa mabao hayo matatu ya Yanga na Simba, maana yake yeye ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi dhidi ya watani wa jadi kwa msimu huu wa 2017-18 na inawezekana ndiye mchezaji hadi sasa amewafunga wakongwe hao mabao mazuri zaidi.
Tukubaliane, Kiyombo ana kitu ambacho sasa kinapaswa kutazamwa na ikiwezekana apate nafasi zaidi. Sisemi hivi nimvimbishe kichwa, badala yake naona ana kitu kinachoweza kumpeleka mbali zaidi.
Kama ingekuwa ni uwezo wangu na ndiye mtu wa mwisho kuamua ningesema huenda vizuri asiende Yanga wala Simba na apitilize tu kama ilivyokuwa kwa Thomas Ulimwengu.
Mbwana Samatta alikaa kidogo Simba, ikampa nafasi ya kusonga. Lakini ninaamini Kiyombo akipata timu kubwa ya nje, ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwa kuwa ana kipaji, ana nia na asiye na hofu ya kufanya utekelezaji.
Kikubwa kabisa kwa Kiyombo anachotakiwa ni kukiendeleza kipaji chake kwa kujifunza na awe makini asivimbe kichwa lakini pia asisikilize miluzi mingi.
Kabla ya kumsifia Kyombo ni wakati muafaka wa kumpa heshima kubwa kocha wa mbao. Ninaimani kabisa kuwa yule kocha wa mbao ni kocha hasa labda tunadharau uwezo wake kwakuwa anatokea Burundi. Huwezi kusifia chakula bila kutambua uwezo wa mpshi. Yule kocha wa mbao ni sawa na almasi ilioko kwenye tope. Ni kocha anaefaa kabisa kupewa majukumu ya timu za taifa hasa timu za vijana. Anaonekana ni mlezi mzuri sana wa kuibua na kukuza vipaji.
ReplyDeleteKwann unapochambua yanga unaficha mabaya yake sema yanga amewafunga mawili sio kusema kwa jumla matatu eti wamefungwa wakongwe
ReplyDelete