Kocha Mkuu wa Mbao FC, Ettiene Ndayiragije raia wa Burundi, amewasifu vijana wake kutokana na kufuata maelekezo yaliyowafanya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga, wikiendi iliyopita.
Katika kuwasifu huko, ameahidi kuendelea kuifunga timu hiyo kila atakapokutana nayo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, uliopo jijini Mwanza.
Ikumbukwe kuwa, Jumapili iliyopita, Mbao iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Hii ni mara ya tatu kwa Yanga kufungwa na Mbao uwanjani hapo, kwani msimu uliopita katika mechi ya ligi kuu, Mbao iliifunga Yanga bao 1-0, kisha ikaibuka tena na ushindi kama huo katika Kombe la FA. Miaka ya nyuma, Yanga ilikuwa na matokeo mazuri uwanjani hapo lakini si dhidi ya Mbao, bali ilipokuwa ikipambana na Toto Africans.
“Siri ya sisi kuwa bora dhidi ya Yanga nadhani ni namna ambavyo vijana wamekuwa wakifuata kile ambacho nimekuwa nikiwaelekeza, si tunapocheza na Yanga tu, bali hata na timu zingine hasa kwenye uwanja wetu wa nyumbani tumekuwa tukifanya vizuri sana.
“Hatutaki kuona tunapoteza mechi hapa kwetu ndiyo maana tumekuwa tukijitahidi sana kucheza kwa juhudi, hata Simba inapokuja huku inapata shida kuondoka na pointi.
“Kama wakiendelea kutudharau kila wakija huku na kujiaminisha kwamba lazima washinde, basi tutakuwa tunawafunga kila siku,” alisema Ndayiragije.
0 COMMENTS:
Post a Comment