Beki kisiki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani anatarajiwa kuikosa mechi ya kesho dhidi ya Ruvu Shooting ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yondani ataikosa mechi hiyo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano alizozipata kwenye mechi zilizopita za ligi kuu.
Kutokana na hali hiyo, timu inaweza kumtumia beki wa kati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ au Said Makapu kucheza nafasi hiyo ya beki ya kati pamoja na Vicent Andrew ‘Dante’.
Taarifa zinaeleza Benchi la Ufundi la Yanga tayari limeanza kuchukua tahadhari ya kuwaandaa baadhi ya wachezaji akiwemo Cannavaro atakayecheza nafasi ya Yondani.
“Yondani ameondolewa kwenye mipango ya kocha katika kuelekea mechi dhidi ya Ruvu itakayochezwa keshokutwa (kesho Jumapili) Uwanja wa Taifa.
“Beki huyo ataukosa mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano alizozipata katika michezo iliyopita ya ligi kuu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Meneja Mkuu wa Yanga, Hafidh Saleh alithibitisha Yondani kuondolewa kikosini; “Ni kweli Yondani hatakuwepo katika mechi dhidi ya Ruvu kwani ana adhabu ya kadi tatu za njano.”
0 COMMENTS:
Post a Comment