Emmanuel Okwi amefikisha mabao 10 na kuzidi kukaa kileleni kwa ufungaji bora mwa Ligi Kuu Bara ambayo sasa inaongozwa na kikosi anachokichezea cha Simba.
Okwi amefikisha mabao 10 baada ya kuongoza kwa muda mrefu akiwa na manane ambayo yamewahangaisha washambuliaji wengi kuyafikia angalau, Habibu Kyombo wa Mbao FC aliyefikisha saba sawa na Mohamed Rashid wa Prisons ambaye amekwama katika idadi hiyo kwa muda mrefu sasa.
Wakati Okwi anafunga mabao hayo mawili, ndiyo alikuwa amerejea nchini kujiunga na Simba siku tatu zilizopita na alifanikiwa kufanya mazoezi kwa siku mbili tu.
Hakuna asiyejua kwamba Okwi amechelewa kurejea kambini hata kama angekuwa na sababu zipi za msingi bado kuna walakini. Ndiyo maana akawaomba radhi walimu wake.
Wakati anaondoka alimuacha Kocha Joseph Omog, lakini amerejea na kukuta akiwa ameshatimuliwa na Simba ikifundishwa na yule msaidizi, Masoud Djuma ambaye hakuwahi kufanya naye kazi akiwa bosi.
Pia ameikuta Simba iko katika hatua za mwisho kumpata kocha mpya, Pierre Georges Lechantre raia wa Ufaransa ambaye alikuwa jukwaani wakati Okwi akifunga mabao mawili Simba ilipoitwanga Singida United kwa mabao 4-0.
Kati yetu hakuna anayeweza kukubaliana na suala la utovu wa nidhamu, hata Okwi kama ana matatizo yake lakini aliporejea ameomba radhi kwa kuwa anaamini kisicho sahihi kinapaswa kujutiwa na kurekebishwa.
Kuomba radhi ni kukubali kurekebisha ulichokosea. Ili arekebishe lazima ajitume na kufanya vizuri na huenda ndiyo hii stori niliyopewa.
Kwamba baada ya Okwi kurejea na kuelezwa wangemkata mshahara, naye aliomba radhi lakini akawaahidi siku chache zijazo watasahau na kusisitiza ataanza kuonyesha katika mechi ya Singida.
Kama hilo ni kweli, maana yake anajitambua. Huenda amekosea kweli lakini anajua Simba wanataka nini naye anaweza kufanya kipi. Kweli hii ni sawa na ile hadithi ya bosi anayetaka kumuona mfanyakazi wake saa zote ofisini lakini hana matunda, japo angeweza kufaidika na mfanyakazi asiyekaa muda mwingi ofisini lakini akawa na faida kubwa.
Naweza nikamtolea mfano mshambuliaji Laudit Mavugo wa Simba ambaye amebaki katika kikosi hicho na anaweza kulalamika kwamba amekuwa hapati muda wa kutosha kucheza ndiyo maana anashindwa kufanya vizuri.
Unakutana na mtu kama Okwi, ambaye anaingia katika dakika ya 65, maana yake alipata dakika 25 tu za kucheza na kufanikiwa kufunga mabao mawili.
Mavugo ambaye ni mshambulizi wa kati, ana mwendo wa kusuasua kupita kiasi. Yupo kwenye timu, anashiriki mazoezi na anapata muda wa kucheza zaidi ya hizo dakika 25 lakini bado kashindwa kuonyesha cheche.
Washambulizi walio Simba wamepata muda wa zaidi ya dakika 25 za Okwi lakini hakuna walichofanya hadi leo, wanajisikiaje? Kama hawakuwa wakiamini muda wanaopata kuutumia ni mali, baada ya kile alichokifanya Okwi wamejifunza nini?
Ukiwa muungwana na unataka kubadilika lazima ukubali matatizo au makosa yako. Naweza kusema, Okwi amekuwa akifanya anavyotaka kwa kuwa anajua ana nafasi kubwa ya kufanya anachotaka kwa kuwa udhaifu mkubwa wa wale anaofanya nao kazi.
Wakati anahojiwa baada ya ushindi wa Singida, alianza kuwashukuru wachezaji wenzake kwa ushirikiano. Hakika hili unaweza kulisikia mara chache kwa wachezaji wa Kitanzania. Mazungumzo yanaonyesha Okwi anajitambua, yanaonyesha ni mchezaji anayejua nini kinatakiwa kufanyika.
Mabao yake mawili yamekuwa muhimu kurudisha morali ya Simba lakini yanamfanya aonekane tofauti hata kama anakosea, bado ni mtendaji bora kuliko wale wenye nidhamu.
Nidhamu inahitajika hili ni muhimu sana, lakini matokeo bora katika nyanja ya kazi ni jambo muhimu zaidi na Okwi anawafundisha, kuwa na nidhamu bila ya matokeo yanayotakiwa, nayo ni kazi bure pia.
Mnaota ndoto za kupiga hatua, hauwezi kufanikiwa kupata timu kubwa zaidi ya Simba kama matokeo yako ni hasi. Kumbuka yakiwa hivyo utakwenda chini, ikiwa ni chanya, utapata timu ya juu zaidi na Okwi ana nafasi ya kwenda, akipenda anarudi kwa kuwa anachofanya katika utendaji wa kasi ni chanya, basi sasa kama mna chanya ya nidhamu, ongezeni na ya utendaji badala ya kuendelea kulala na kulalama.
0 COMMENTS:
Post a Comment