Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Hemed Morocco, amefunguka juu ya kutakiwa na timu ya DC Motema Pembe ya DR Congo ambayo inahitaji huduma yake msimu ujao huku timu kadhaa kutoka nje zikionyesha nia ya kumuhitaji pia.
Morocco ambaye aliiongoza Zanzibar Heroes katika michuano ya Chalenji nchini Kenya, mwaka jana na kufanikiwa kutwaa nafasi ya pili ya michuano hiyo kwa kutolewa na timu ya taifa ya Kenya katika hatua ya fainali, amekuwa akipata ofa nyingi ndani na nje ya nchi kutokana na uwezo wake aliouonyesha katika michuano hiyo.
Morocco amesema kuwa timu mbalimbali zimekuwa zikimhitaji kwa lengo la kuzifundisha msimu ujao kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo DC Motema Pembe timu ambayo aliwahi kuichezea aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan Mgosi.
“Nitarudi kwenye gemu msimu ujao, kuna timu nyingi ambazo zinanihitaji hivi sasa ikiwemo DC Motema Pembe lakini bado sijafanya mazungumzo nao, pia nimepokea ofa nyingi kutoka nje na Tanzania Bara lakini ni mapema mno kuzitaja timu zinazonihitaji.
“Timu nyingine ambazo zinanihitaji zinatoka Congo, Uganda na Sudan huko kote kuna timu ambazo zinanihitaji nitaziweka wazi hadi tutakapofikia makubaliano na moja wapo,” alisema Morocco.
0 COMMENTS:
Post a Comment