INAWEZEKANA MBAO TUKAIPA MKONO WA KWAHERI BAADA YA MSIMU HUU LIGI KUU BARA
Na George Mganga
Ukiachilia mbali Majimaji, Njombe Mji na Kagera Sugar, Klabu ya Mbao FC nayo imekuwa moja ya timu zinazopambana kuepuka kushuka daraja msimu huu.
Licha ya kuonesha upinzani mkubwa haswa pale inapokutana na klabu zenye majina kwenye Ligi Kuu Bara, Mbao FC imekuwa na mwenendo mbaya zaidi msimu huu.
Katika msimu wa ligi uliopita, timu hiyo ilinusurika kushuka daraja kwenye dakika za mwisho kabisa, ilipocheza dhidi ya Yanga pale CCM Kirumba.
Pengine hata msimu huu tusingekuwa nayo kwenye ligi kutokana na ushindi walioupata wa bao 1-0 dhidi ya Yanga ikiwa ni May 7 2017 na kuwabakisha kwenye ligi.
Baada ya kupanda ligi msimu wa 2016/17, Mbao ilileta changamoto kubwa na pengine kuaminiwa na wadau wa Mwanza inaweza kuutangaza mkoa huo vizuri kisoka.
Ukiachana na Toto Africans ambayo imekuwa ikipanda na haikai zaidi ya misimu miwili kwa miaka ya hivi karibuni, Mbao ilipewa nafasi ya kufanya vizuri kutokana na mwanzo wao namna ulivyokuwa.
Lakini ukiutazama msimamo wa Ligi namna ulivyo, klabu hiyo ipo kwenye nafasi ya 13 ikiwa imeshacheza jumla ya michezo 22 na ikiwa ina pointi 19.
kwa muda mrefu mkoa wa Mwanza ulikuwa na Toto Africans kama timu pekee iliyowakilisha katika Ligi, ila imekuja kufeli kutokana na siasa za Uyanga na Usimba kuingia ndani yake.
Ujio wa Mbao ulidhaniwa labda unaweza ukaondoa usiasa huo uliokuwa umeshamiri kwa Toto Africans, lakini mwenendo wa timu hiyo kupitia kwa viongozi kwa ujumla unaweza ukatoa mkono wa 'Byebye' kwenye ligi kama kama wasipobadilika.
Tunajua asilimia ya timu nyingi hapa nchini zimekuwa zikiyumba kutokana na kukosa wawekezaji, kwa maana mpira bila pesa haziendi.
Mpaka leo hii ni Yanga, Azam, Simba pamoja na Singida United iliyopanda daraja msimu uliopita zinauwezo wa kupanda ndege kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Nje ya hivyo, bado vingine vipo kwenye hali ngumu.
Ni muda mwafaka wa viongozi wa mkoa wa Mwanza kukaa chini na kujitafakari kuangalia mbadala wa tatizo. Heshima ya Mwanza ilijengwa na Pamba.
Lakini heshima hiyo haipaswi kutelekezwa hivihivi, badala yake kunapaswa kuwepo mipango na mikakati madhubuti ya kuirejesha tena.
Kubwa zaidi ni kuweka pembeni siasa kwenye mpira, haviambatani hata siku moja.








0 COMMENTS:
Post a Comment