March 23, 2018








Na Saleh Ally
WAKATI nikiwa jijini Cairo nchini Misri kujiandaa na safari ya kurejea nchini, nilipata nafasi ya kuishuhudia mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji Zamalek dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia.

Sikupata nafasi ya kwenda uwanjani baada ya kuonekana hakukuwa na muda wa kutosha licha ya kwamba mechi hiyo ilikuwa ikichezwa palepale Cairo.

Nilikuwa katika msafara wa Simba waliokuwa wanarejea nyumbani baada ya kutolewa na Al Masry ambayo makao yake ni katika Mji wa Port Said ulio Kaskazini Mashariki mwa Misri.

Uamuzi ulikuwa ni kuangalia kwenye runinga, mimi pamoja na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini humo. Wengi waliamini nafasi ya Zamalek kufuzu ilikuwa kubwa sana licha ya kwamba Dicha walishinda katika mechi ya kwanza kwa mabao 2-1. Wengi waliiamini Zamalek kwamba ingeweza kupindua matokeo.

Ilikuwa inakutana na timu ya kawaida kabisa ambayo ni maskini huwezi kuilinganisha na Zamalek kifedha, umaarufu au rekodi.

Hata katika ligi ya kwao, Dicha wako katika nafasi ya nane, hivyo yeyote aliyekuwa akiamini Zamalek ina nafasi ya mchekea, alikuwa sahihi ingawa katika soka, ni sahihi kufanya tathmini ya kutosha.

Dicha inatokea katika mji mdogo wa Wolaita Sodo na uwanja wake wa Wolaita Soddo una uwezo wa kubeba watu 10,000 tu. Hakika ni mbaya na haufai kuchezewa mechi za kimataifa, ndiyo maana wanalazimika kucheza jijini Awassa.

Ni timu inayoundwa na wenyeji wasio na majina makubwa lakini wana uwezo. Wana wageni watatu tu ambao ni kipa Mnigeria, Emmanuel Obhyo, Kiliouto Massama kutoka Chad na raia wa Togo, Arafat Djako, mmoja wa washambulizi hatari.

Pamoja na udogo wao, Dicha waliopambana na mwisho wakawa wamepoteza kwa mabao 2-1 jijini Cairo, sawa na ushindi walioupata wao kwao Ethiopia. Wakaenda kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti na kuibuka na ushindi wa mikwaju 4-3. Kigogo akaangukia pua.

Sasa wanakutana na Yanga na ndiyo gumzo kubwa kutokana na taswira inayotengeneza mwonekano sahihi wa Dicha ambayo inachanganya.


Huenda kukawa na maswali mengi zaidi ya kujiuliza kuhusiana na Dicha kutokana na taswira yake kutokuwa imeshikilia sahihi kumfanya mtu aweze kuwatafsiri kirahisi.

Hakika ni timu ngumu kukutana nayo kuliko Yanga au wapenda soka wanavyofikiria na inawezekana ikawa nafasi nzuri ya Yanga kufika mbali na kuingia hatua ya makundi kama wataiona Dicha ni timu nzuri inayopaswa kufanyiwa maandalizi sahihi na ya uhakika kwa kuwa si timu ya mzaha kama ulivyo muonekano wake wa nje.

Yanga inaweza kujiuliza maswali haya matano ya kuyafanyia kazi kwa Dicha na kinachotakiwa ni kupambana na kuivuka na kwenda katika makundi ambako kuna utajiri na biashara nzuri kwa kuwa itajitangaza na ikiwezekana kuuza wachezaji wake.

MOJA:
Yanga imejifunza kilichoitokea kwa Township Rollers, ilikuwa ni timu inayokutana na Yanga baada ya kuitoa timu ngumu ya Waarabu wa Sudan, El Merreikh.

Inaonekana Yanga hawakujiandaa kabisa kwa mechi ya kwanza nyumbani na huenda waliamini mambo yangekuwa rahisi, yakawa magumu kuliko walivyotarajia. Je, wanajua Dicha imewatoa Waarabu wa Misri? Vizuri kujiandaa na hakuna mzaha.

MBILI:
Yanga lazima waamini hadi wanashuka kutoka Ligi ya Mabingwa, moja ya timu walizozikuta katika Kombe la Shirikisho ni Dicha. Tena wanaikuta baada ya kuitoa Zamalek. Je, nani anaweza kusema hiyo ni timu ya kubeza?

TATU:
Tayari mechi yao dhidi ya Rollers imewafunza Yanga lakini ile kati ya Dicha na Zamalek inaonyesha ushindi wa mabao mengi ni mzuri kwa kuwa Dicha wana uwezo mkubwa wa kulinda wakiwa ugenini kwa kuwa wamefungwa mabao 2-1 na Zamalek.

NNE:
Yanga wana uwezo wa kupigana linapofikia suala la mikwaju ya penalti? Kama kuna shida kidogo lazima wajue Dicha ni wakali na hawapaswi kuwafikisha huko, dawa yao ni kumalizana nao mapema katika dakika 90 mara mbili za mechi ya kwanza na ya pili.

TANO:
Sijui kama Yanga wanajua, Dicha wana utajiri wa mioyo maana matokeo yao hayatishi na hata kwenye ligi wako nafasi ya nane lakini wameweza kuitoa Zamalek.

Kama hiyo haitoshi, Yanga wapige hesabu hii, kwamba pamoja na umasikini huo licha ya kuwepo kwa timu kubwa kama St George au Dedebit, Dicha bado walikuwa mabingwa wa Kombe la Ethiopia na kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni timu changa iliyoanzishwa mwaka 2009 tu, lakini kama wameweza kubeba ubingwa kwao Ethiopia basi si wa kubeza na lazima Yanga wajue wanakutana na wanajeshi wasiokuwa na sura moja.

Yanga ikijiandaa inaweza kufanya vema na historia pia inaipa nafasi kwa timu za Ethiopia, maana miaka 19 na ushee, Yanga ilikutana na Coffee ya Ethiopia na kuing’oa katika michuano ikafanikiwa kutinga makundi.

Wakati Yanga inakutana na Coffee, timu hiyo ya Ethiopia ilikuwa imetoka kuing’oa Zamalek ya Misri na ilionekana ni kama miujiza. Hivyo isingekuwa jambo rahisi Yanga kuitoa timu iliyoitoa Zamalek.

Umakini ulioongezeka kutokana na namna timu iliyokuwa inakutana nayo kuonekana ngumu, ndicho kilichoisaidia Yanga kufanya vema na kuendelea kubaki na rekodi hiyo ya juu hadi leo. Maana yake, hata sasa inawezekana na ugumu wa Dicha utumike kama sehemu ya ubora wa maandalizi ya Yanga.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic