March 23, 2018




NA SALEH ALLY
KUNA mabadiliko makubwa yanatakiwa kuendelea kupatikana ili kutengeneza timu bora ya taifa letu.

Taifa Stars imekuwa ni timu inayosuasua lakini haitabadilika kama mambo yataendelea kuwa yalivyo katika kipindi hiki.

Kuna mengi yanapaswa kufanyika likiwemo suala la kukuza vipaji zaidi na kuviendeleza ili kuwa na wachezaji waliokulia katika misingi sahihi ya mchezo wa soka.

Wanaoandaliwa mapema wanaweza kuwa msaada mkubwa baadaye hasa kama maandalizi yao yanafuata mfumo sahihi wa uzalishaji.

Lazima kuwe na vitu sahihi kupitia mfumo ulio sahihi pia kuwakuza wachezaji na itakuwa vizuri kama mfumo huo pia ukatengenezwa katika ngazi ya klabu.

Kwa kuwa lengo letu ni kutengeneza timu bora na sahihi ya taifa, lazima pia tukubali katika plani za muda mfupi, suala la kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania ni muhimu.

Wachezaji wanaokuwa nje ya Tanzania wanapoongezeka, unazidi kuongeza uhakika wa mambo ndani ya simu au hamasa ambayo itasaidia kuongeza mambo muhimu kadhaa.

Mchezaji anayetokea nje ya Tanzania anaweza kuwa anajitambua kwa mengi, mfano lile la mchango wake katika timu kwa kuwa anaijua thamani ya kuchaguliwa katika kikosi.

Yule anayecheza nje anakuwa anajua thamani ya timu ya taifa kwa kuwa kama itafanikiwa kucheza Kombe la Mataifa Afrika au Kombe la Dunia ni faida kubwa kwake kuliko kuzikosa nafasi hizo.

Mchezaji anayetokea nje ya nchi kurejea kucheza nyumbani anakuwa amejifunza mengi kuhusiana na mchezo wa soka kuliko aliye nyumbani.

Suala la nidhamu kwake linakuwa ni namba moja na anajua nini cha kufanya. Kuwa na nidhamu ya juu ni utambuzi wa wewe binafsi na hii inasaidia kuongeza utendaji uliotukuka.

Mchezaji anapokuwa na utendaji bora maana yake msaada wake katika kikosi unapanda kwa zaidi ya asilimia 90. Hii inamaanisha timu inainuka kiwango na uhakika wa kufanya vizuri pia unakuwa kwa zaidi ya asilimia 75.

 Kama tutaamini wachezaji wa Kitanzania wakicheza kwa wingi nje watakuwa msaada basi kuna kila sababu ya kuhamasisha wachezaji zaidi kujitoa na kwenda nje.

Tunajua watatakiwa kujituma kupata nafasi za kucheza nje na watatakiwa kuwa na nidhamu ya juu ili kucheza nje ya Tanzania.

Lakini kuna jambo ambalo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), pia linapaswa kulipa kipaumbele ili wale waliopata nafasi za kucheza nje hata kama zinaonekana ni chache, lazima wawafuatilie kwa karibu na kujua maendeleo yao.

Kujua maendeleo yao ni jambo sahihi na wajibu wa TFF kwa kuwa ndiyo mara nyingi inawatumia katika kikosi hicho cha taifa.

Kuwafuatilia kwa ukaribu kwa lengo la kujua viwango vyao na wanaendeleaje kama wachezaji wa timu ya taifa, ni jambo zuri sana na linatakiwa kufanyika kama sehemu ya uangalizi ya kinachoendelea.

Lazima TFF kupitia wataalamu wake iwe na uhakika wachezaji hao wako wapi, wanachezea timu gani na nafasi zao za kucheza ni kiasi gani.

TFF lazima ijue taarifa za uhakika, iwe na ukaribu na timu zao na mawasiliano ya karibu kufuatilia maendeleo yao na hili ni muhimu sana kwa Tanzania.

Kwa sasa Tanzania haina wachezaji wengi wanaocheza nje ya Tanzania. Kama ufuatiliaji utakuwa wa karibu itakuwa kazi rahisi hata kwa walimu wa timu za taifa kujua wanafanya nini.

Lakini ukaribu na timu wanazozichezea unasaidia uhusiano wa karibu kati ya shirikisho na kwingine kulikopiga hatua kisoka. Pia kujua wengi ambao wamekuwa wakielezwa wanacheza nje lakini hawakuwahi kucheza Tanzania kabla.

SOURCE: CHAMPIONI




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic