Kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Tip Top Connection, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ na Meneja wa Diamond Platnumz dhidi ya Shehe Salum Mbonde bado inaonekana ni ngoma nzito baada ya wawili hao kuitwa tena mahakamani kwa ajili ya kupitiwa tena kwa kesi yao.
Babu Tale, akisimama kwa niaba ya wamiliki wa Tip Top Conection, alishitakiwa na shehe huyo kwa madai ya kudurufu ‘CD’ za mawaidha za Shehe Mbonde na baadaye mahakama ilitoa uamuzi kwamba Babu Tale, amlipe fidia mlalamikaji ya shilingi milioni 250 kwa kosa hilo.
Shehe Mbonde alisema kwamba, waliitwa Mahakama Kuu Tanzania Juni 8, na Jaji Edson Mkasimongwa, ambaye alimtaka wakili wake Mwesigwa Mhingo kuieleza mahakama historia nzima ya kesi hiyo.
“Wakili wangu alisimulia juu ya kesi hiyo yote mpaka hukumu yake, ambapo baada ya kumaliza upande wa mshitakiwa (Babu Tale), waliibua hoja kwamba aliyetoa hukumu ya kesi hiyo Jaji Augustine, alikwisha staafu na alisaini hukumu hiyo wakati akiwa ni mstaafu.
“Lakini hoja nyingine ambayo waliibua upande huo wa pili ni kwamba, Msajili wa Mahakama Kuu, Mashauri ambaye alitoa hukumu ya kesi hiyo, hana mamlaka kisheria kumpeleka jela mtuhumiwa wa kesi ya madai,” alidai Shehe Mbonde.
Shehe huyo aliendelea kusimulia kwamba, hata hivyo hoja ya kwanza ilijibiwa na mahakama kwamba hakukuwa na tatizo lolote kwa jaji Augustine kusaini hukumu yake akiwa amestaafu au la, kwani kama alianza nayo kabla hajastaafu alikuwa ana uwezo wa kuimaliza hata alipostaafu.
“Kwa hiyo mahakama ilitupilia mbali hoja hiyo ya kwanza kwani Jaji Mkasimongwa, hayupo kwa ajili ya kutengua hukumu iliyotolewa na jaji mwingine,” alisema Shehe Mbonde.
Aliendelea kueleza kwamba; “Kwa upande wa hoja ya pili, wakili wangu aliibua vifungu vya sheria vilivyoonyesha kwamba msajili ana mamlaka ya kumpeleka jela mtuhumiwa wa kesi ya madai.”
Shehe huyo alimaliza kwa kueleza kuwa baada ya mvutano mkubwa mahakamani, mahakama ilipanga pande zote mbili kukutana mahakamani Jumatatu ya Juni 25 mwaka huu.
CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS
0 COMMENTS:
Post a Comment