NA SALEH ALLY
MABINGWA wa soka Tanzania, Simba wameamua kuelekeza nguvu zao katika michuano ya Kombe la Kagame ambayo itafanyika ndani ya siku chache zijazo.
Wapinzani wao wakubwa Yanga waliokuwa nao kundi moja, wamejitoa na kutangaza sababu zao ikiwemo wakati “mbaya” kwao michuano hii kufanyika kipindi hiki lakini kuwa katika michuano ya kimataifa.
Yanga ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa maana kwa sasa wanashiriki Kombe la Shirikisho hatua ya makundi.
Simba, Azam na Singida United wanatokea Tanzania Bara na wanajua kutakuwa na timu za Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na kila mmoja atataka kombe hilo.
Wakati Simba wanaingia kushiriki kombe hilo, wanajua kuwa wao watakuwa wanatazamwa zaidi kutokana na kwamba ndiyo timu kubwa itakuwa imebaki katika michuano hiyo.
Lakini Simba wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kuingia fainali kikanda katika michuano ya Kombe la SportPesa Super Cup ambayo walistahili kufanya vema zaidi kama wangekuwa makini.
Huenda Simba wamekuwa wakichukulia vitu “poa tu” lakini mashindano ya kimataifa ni jambo linalojumuisha ushindi na heshima kuanzia ngazi ya klabu hadi taifa. Maana yake haliwezi kuwa jambo la kufanyiwa mzaha.
Yanga wamefanya uamuzi wa kuondoka mapema, Simba kama wamebaki basi hawana ujanja ni lazima wafanye vizuri na hasa kwa kuwa mashindano hayo yatakuwa yanafanyika katika ardhi ya Tanzania.
Ninaamini watakuwa wamejiandaa ili kuepusha kuendelea kuumiza mioyo ya mashabiki na wanachama wao kwa kuwa timu imepumzishwa na kama ni hivyo basi inayoshiriki lazima iwe makini na yenye ushindani inayotaka kushinda.
Kama unakumbuka kwa sasa timu anayo Kocha Msaidizi, Masoud Djuma ambaye aliwahi kuachiwa timu kwa muda kabla ya ujio wa Mfaransa, Pierre Lechantre na akafanikiwa kushinda mechi mbili mfululizo za ligi ikiwa gia mpya Simba kuanza kusaka ubingwa “wenye uchungu”.
Huu ni wakati mzuri zaidi kwa Djuma na Simba, unakuwa wakati mzuri kwa kuwa yeye atakuwa na nafasi ya kuonyesha alichonacho na ikiwezekana akawabadili mawazo waajiri wake kwamba hawana sababu ya kuleta mtu mwingine katika nafasi yake.
Lakini pia ni wakati mzuri kwa uongozi wa Simba kumuona vizuri Djuma kwa kuwa alipata muda mchache baada ya kuondoka kwa Joseph Omog na kutua kwa Lechantre. Huenda itakuwa vigumu kuuamini uwezo wa Djuma kwa kipindi hicho kifupi.
Kwa kuwa sasa muda unatosha, basi kila mmoja anatakiwa amuamini mwenzake na kufanya kila kinachowezekana kifanikiwe. Na kama kila upande utafanikiwa kumtekelezea mwenzake basi kila upande utafanya vema.
Wanachotakiwa Simba kwa sasa ni kumpa kocha huyo Mrundi msaada au ukaribu wa hali na mali ambao atakuwa anahitaji kwao na ikiwezekana ile heshima ya Lechantre basi waihamishie kwamba huyo ndiye kocha wao na anahitaji msaada wa kile wanachokiweza ili kufanikisha kazi zao sahihi.
Nafasi ya kocha mkuu si jambo geni kwa Djuma maana amechukua ubingwa wa Rwanda na makombe mengine akiwa na Rayon Sports na alikuwa mmoja wa makocha waliofanya kazi yao kwa ufasaha kabisa.
Hii maana yake, hawezi kushindwa jambo na hawezi kuwa mgeni na ushindani wa aina hiyo na kama alifanikiwa na Rayon ambayo ina presha kubwa aina ya Simba, basi anaweza kufanikiwa hapa kama ataungwa mkono.
Hivyo, Simba wanapaswa kumuamini Djuma na kumsaidia ili waione nguvu ya kazi yake katika wakati sahihi na baada ya hapo wataweza kumtathimini zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment