July 7, 2018


Bilionea wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ amedaiwa kuchelewesha mkataba wa kocha anayetajwa kuanza kuinoa timu hiyo kwa kuchukua mikoba ya Mfaransa, Pierre Lechantre.

Jumapili iliyopita, uongozi wa Simba unadaiwa kumshusha nchini, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji kwa ajili ya kuwa kocha mkuu wa timu hiyo baada ya hivi karibuni Lechantre kufungashiwa virago vyake klabuni hapo.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumamosi limezipata zimedai kuwa Aussems angekuwa tayari ameishapewa mkataba wa kuinoa timu hiyo lakini zoezi hilo limekwama kutokana na kile kilichodaiwa Mo kuwa safarini.

Kutokana na hali hiyo, kocha huyo imemlazimu asubiri mpaka bilionea huyo atakaporejea nchini.

“Mpaka sasa Aussems hajapewa mkataba wowote kutokana na Mo kuwa safarini kwa hiyo hakuna ambacho kimefanyika mpaka sasa.

“Labda muda wowote kuanzia leo kama Mo atakuwa amesharudi nchini basi ndipo anaweza kupatiwa mkataba wa kuinoa timu yetu,’ kilisema chanzo hicho cha habari.

Walipotafutwa viongozi wa Simba ili waweze kulizungumzia hilo hakuna aliyekuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai kuwa hawana taarifa juu ya kocha huyo.

Hata hivyo, Kocha huyo ambaye tayari amefanikiwa kukiona uwanjani mara mbili kikosi cha Simba katika michuano ya Kombe la Kagame kikicheza dhidi ya APR pamoja na Singida United lakini hakutaka kuweka wazi mpango wake huo wa kutaka kujiunga na Simba.

CHANZO: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV