July 4, 2018




Straika mpya wa Simba, Meddie Kagere, ameeleza ‘umafia’ ambao Simba waliutumia mpaka kuinasa saini yake bila ya timu yake kujua chochote, huku akiwakana Yanga.

Kagere ambaye mapema wiki iliyopita alikamilisha usajili wake wa kujiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Gor Mahia ya Kenya, juzi Jumatatu alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na jezi za Simba ikiwa ni siku moja baada ya kuanza mazoezi na wenzake.

Katika mchezo huo wa Kombe la Kagame uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya APR ya Rwanda, Kagere alifunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti.

Ikumbukwe kuwa, wakati Kagere amekuja Tanzania kumalizana na Simba, hakukuwa na kiongozi yeyote wa Gor Mahia aliyekuwa akijua hilo zaidi ya wakala wake, Patrick Gakumba na yeye mwenyewe jambo ambalo linatajwa ni umafia ulifanyika.

Kagere alisema: “Unajua mimi nilikuwa tayari nimemaliza mkataba wangu na Gor Mahia, sasa nilikuwa nasubiri nipewe mkataba mpya, lakini kwa muda mrefu wakawa kimya licha ya kuwaambia jambo hilo. Nikaona kama vile hawanihitaji.

“Simba waliponifuata nikazungumza nao na nikawaeleza kwamba sikuwa na mkataba, wakaniwekea maslahi mazuri zaidi, haraka sana nikaamua kujiunga kwao kwa sababu niliona wao ndiyo wanaihitaji huduma yangu kuliko nilipokuwepo.

“Hivi sasa mimi ni mchezaji wa Simba na nimeondoka Gor Mahia nikiwa sina deni kwa sababu sina mkataba nao. Kwa sasa akili yangu yote ipo Simba na si kwingine.

Alipoulizwa kuhusiana na tetesi za awali kuwa alitakiwa na Yanga kabla ya kwenda Simba alisema ” Yanga hapana, ukweli hawakuwahi kuzungumza nami,” alisema staa huyo.

Usajili wa Kagere ndani ya Simba, unatajwa kuwa ni Sh milioni 115, huku mshahara wake wa mwezi ukiwa ni Sh milioni 12.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic