August 17, 2018

ROSTAM


NA SALEH ALLY
NIMELALAMIKA sana kuhusiana na suala la viongozi wengi wanaofanya kazi katika ngazi mbalimbali zinazosimamia watu kuwa wabunifu badala ya kutaka kufanya waonekane au kusikika!

Wako ambao wamekuwa wakinielewa na baadhi kuona kama nawashambulia lakini hakika suala la viongozi wanaohudumia watu kutaka waonekane wamefanya vizuri limezidi kukua.

Nimeona wengi wanafanya hivyo ili waonekane kwa wakubwa na kujihakikishia ajira zao kwa kuwa wanaamini wakifanya bila ya kelele, huenda wataonekana hawafanyi kazi. Hili ni jambo jingine baya sana.

Binafsi nakerwa na viongozi wanaofanya kazi kufurahisha baadhi huku wakijua wanawaumiza watu na nitaendelea kukemea hili na safari hii nikianza na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Basata ndiye baba wa sanaa nchi hii, lakini inaonekana wazi wamekuwa wakifanya uamuzi wao mwingi katika ile hali inaonekana ni waoga na wamepanga kufanya mambo yao kutaka kuonekana wamefanya.

Nimeona adhabu zimekuwa zikitolewa mfululizo kwa wasanii na hakika nyingine zimekuwa hazina mashiko, huenda ni kwa kuwa viongozi wa Basata nao wangependa kuonekana wamefanya jambo.

Watu wengi wamekaa kimya pamoja na Basata kuendelea kufanya uamuzi ambao binafsi naona umekuwa si sahihi. Inaonekana wengi wangeweza kuzungumza na kuweka maoni yao hadharani, lakini uoga wa kuamini Serikali haitaki kukosolewa, jambo ambalo binafsi siamini kama ni kweli.

Serikali ingependa itumikie wananchi vizuri na kama Basata wanakosea, bila ya kuweka maoni na ikiwezekana nao wakajirekebisha, lini watakuwa bora?

Mfano, wimbo wa Parapanda wa “Rostam”, yaani Roma na Stamina, una tatizo gani. Basata inapaswa kuweka vitu wazi tatizo hasa la wimbo huo ni lipi! Binafsi nilijaribu kuusikiliza mara nne mfululizo ili kupata jibu, sikuona tatizo.

Basata kama imewaita Roma na Stamina, halafu haitaki kusema kwa jamii kwa madai kwamba wao wanajua wanatakiwa warekebishe wapi, nafikiri si sahihi kwa kuwa kama wanajamii, tungependa kujua au hata wasanii walipaswa kujua ili kujifunza.

Rostam wamekuwa wabunifu, wameimba mmoja akiwa marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na mwingine, marehemu Kingunge Ngombale Mwilu wakiwa kama ndiyo wanakutana mara ya kwanza.

Mwalimu Nyerere akionekana kuuliza maswali mengi ambayo baadhi Kingunge aliyajibu na mengine kuonekana kumshinda. Sanaa iliyotumika inaonyesha kipaji walichonacho tena kwa heshima kubwa.

Nilijiuliza mengi sana kuhusiana na kosa ambalo nalo halionekani. Basata inaona kila wimbo lazima ikosoe? Haipendi viongozi watajwe? Kama ni hivyo ule Wimbo wa Mgunga Mwa Mnyenyelwa ungetoka leo, ninaamini nao ungefungiwa hasa kwa Basata ya sasa.

Angalia ada, msanii anajisajili hadi kwa Sh milioni moja, wakati hana hata fedha Sh laki tano kwa ajili ya kurekodi wimbo wa Sh milioni moja ya kurekodi video! Wakati wasanii wanapambana kupata matangazo, Basata ndiyo inawawekea kauzibe kabisa.

Maana imetangaza gharama za wasanii watakaotumiwa na makampuni, hasa kwenye suala la kujitangaza au branding. Kampuni itakayofanya hivyo itatozwa gharama ya Sh laki 5 na kama ni tangazo kila tangazo la msanii litalipiwa Sh milioni 5.

Binafsi naona ni kitu cha ajabu sana na inaonyesha kiasi gani Basata isivyokuwa na washauri wazuri na huenda wanafurahia kuonekana wanafanya kazi lakini uhalisia wanakuwa sawa na si wataalamu wa sanaa.

Baraza lina msaada gani kuweka mazingira msanii aweze kupata matangazo. Kama amepata tangazo, angalau alifanye kwa bei poa hata Sh milioni moja ili aanze kutambulika haraka. Vipi kampuni ilipe Sh milioni 5 kwa Basata, yaani Basata inachukua fedha hizo kwa ajili gani?

Kama makampuni hayana uwezo wa kutoa hata Sh milioni mbili, na inawezekana wasanii wanaweza kukubali angalau kiasi kidogo ili kujenga imani kwa makampuni ambayo hayana imani nao.

Sasa kampuni itampa msanii kiasi gani kama inatoa Sh milioni 5 kwa Basata? Kwa nini Basata inataka fungu lote hilo kubwa na imewahi kufanya nini kuwasaidia wasanii kupaa na kuaminika?

Basata inafanya nini kuongeza ushawishi na kama usimamizi ndiyo huu wa kutoza fedha pekee kufuta nyimbo zao. Vizuri Basata ikajichukulia kama mzazi, ikajichukulia kama sehemu ya wataalamu ambao wanaweza kuiongoza serikali kufanya mambo sahihi na si kufanya kwa lengo la kuonyesha huku ikizidi kuwaumiza wasanii.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic