August 16, 2018


Kwa mpenzi wa burudani na shabiki wa Muziki wa Hip Hop Bongo hasa wa mwanamuziki Fareed Kubanda ‘Fid Q’, wimbo wake mpya uitwao Kiberiti aliomshirikisha Saida Karoli, mbali na kutoa burudani upande wake wa pili unasikitisha.

Unasikitisha kwa sababu ukiwa unasikiliza wimbo huo wakati una ‘enjoy’ vumbi la kiki, snea na vinanda utagundua Fid Q ameimba akiwa mwenye hasira, kuanzia ‘tone’ ya sauti yake mpaka ujumbe wa wimbo wenyewe! Bila shaka kuna mengi yanamuumiza kwenye ‘career’ yake na ndiyo amejaribu kuyaelezea kupitia wimbo huu. Nakuchambulia kwa kina;

YUPO KWENYE GEMU MUDA MREFU NA ANAPITWA!

Fid Q anatambua kwamba ni mkali na mwenye mashabiki wengi. Lakini asiye na heshima anayostahili. Ndiyo maana kwenye wimbo huu anapomuelezea mtu aliyemvika uhusika kufikisha ujumbe ambapo wazi ninaona alikuwa anajizungumzia mwenyewe anasema kwamba haonekani BET au MTV akitajwa na ni msanii wa muda mrefu anacheza tu!

Wengi wamemkuta kwenye gemu na wameondoka yuko palepale. Akitoa ngoma ni ‘hit song’ Bongo, lakini haifiki mbali zaidi wala hatajwi kwenye tuzo kubwa. Anajilinganisha na wanamuziki wengine ambao wamekuja baada yake na kufika mbali na ndiyo maana anajiona kwamba kwenye gemu anacheza.

LEGEZA KA’ WENZAKO ACHA KUTUKUZA MISEMO

Mstari huu unaonyesha kwamba kuna mengi yanagonga kichwani kwake kama sababu ya yeye kuwa alipo. Ndiyo maana kaandika mistari hii kwamba; “Tatizo lako hutaki kuuza maneno, legeza ka’ wenzako acha kutukuza misemo.” Fid Q anaona pengine sababu za kumfanya asifanye vizuri na kufika mbali ni aina yake ya uimbaji ya mistari ya kumfikirisha mtu.

IKICHORWA HIP HOP SIONI SURA YAKO KWA PICHA

Hapa inaonesha kwamba ndani au nje ya Bongo, wanaweza kuzungumziwa wanamuziki wakali wa Hip Hop Bongo na yeye asiwekwe kwenye listi.

Lakini kwenye listi hiyo wakawemo kina Bill Nas, Rosa Ree na wanamuziki wengine wa kileo na akaachwa yeye ambaye amekuwepo kabla na anakimbizana nao kwa sasa kwenye gemu na pengine yupo juu hata zaidi yao ukilinganisha kazi zao.

HUJAWAHI PIGIWA BUU UNAJIONA 2PAC Nimewahi kushuhudia Fid Q anaposhika kinasa sauti shangwe analoamsha si la kitoto. Si kwa nyimbo zake mpya tu, kuanzia nyimbo zake za mwanzoni alizotoa. Ni ukweli kwamba, hajawahi kupigiwa ‘buu’ lakini hii inatosha kujiona kwamba ana heshima kama ilivyokuwa kwa mwanamuziki kutoka Marekani, marehemu 2Pac Shakur!

AU TUPISHE USAHAULIKE, URUDI KUUZA MITUMBA LANGO

Fid Q amewahi kueleza mara kadhaa kwenye historia ya maisha yake kwamba kabla ya kutoka aliwahi kuuza mitumba kwenye Soko la Langolango.

Kwa wakazi wa Jiji la ‘Rock City’ Mwanza au mtu aliyetembea jiji hilo ambalo a.k.a yake siku hizi ni ‘Rap City’ watakuwa wamefika kwenye soko hili au wamesikia juu ya soko hili. Hili ni kama lilivyo Soko la Karume kwa upande wa mitumba. Alikuwa pale enzi hizo, sasa Fid Q anawaza kwa namna ‘career’ yake ilivyo apige chini muziki na arudi alikotoka?

ANAHITAJI UPENDO

Pengine uzalendo umemshinda na anahitaji ufike wakati aonyeshwe upendo na heshima aliyonayo. Siyo tu kwenye mistari yake mingi inayovutia na kufurahisha watu kama ilivyo rangi ya mistari ya pun-dam-ilia lakini hana heshima kama ya Ali Kiba ‘King- Kiba’ ambaye kwa namna moja au nyingine kuna watu wanamtambua kama mfalme wa Bongo Fleva.

Katika kufikisha hili, Fid Q amesampo baadhi ya mistari ya wimbo wa LL Cool J uitwao I Need Love alioutoa mwaka 1987.

Ukweli ni kwamba kuna mengi unaweza kuzungumzia kuhusu wimbo huu ukiusikiliza kwa makini. Itoshe tu kusema kwamba Fid Q anahitaji sapoti na heshima anayostahili, kweli ni mwanamuziki mkali na mwenye heshima yake.

Baraza la Sanaa (Basata) linaweza kufanya kitu kwa ajili yake. Ukijiuliza ni wanamuziki wa ngapi wa Hip Hop au Bongo Fleva wamepita kwa kufanya vizuri na mwisho wakaishia kupotosha kwa matumizi ya dawa za kulevya na vitu vingine vya ajabu, hakika ni wengi. Lakini Fid Q ameendelea kufanya anachokifanya. Amewavutia na kuwahamasisha vijana wengi kufanya Muziki wa Hip Hop.

Mbali na hayo yote anawasaidia vijana kutambua athari za dawa za kulevya na kuachana nazo. Kama Umoja wa Nchi za Ulaya EU uliutambua mchango wake na kumpa tuzo mwaka 2015 ya Champion of the 2015 Europe Year for Development in Tanzania, vipi kuhusu hapa nchini? Tusapoti vya kwetu na tumsapoti Fid Q

Na Boniphace Ngumije

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic