MTIBWA WAJA NA MBINU MBADALA YA KUMALIZANA NA SANTOS JUU YA DOLA 1500 WASHIRIKI CAF
Imeripotiwa kuwa uongozi wa klabu ya Mtibwa Sugar upo katika harakati za kufanya mazungumzo na Santos FC inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini ili kuwalipa deni lao.
Mtibwa Sugar wanapaswa kuwalipa Santos kiasi cha dola za kimarekani 1500 kutokana na kushindwa kucheza nao mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2004.
Ili kumaliza deni hilo, uongozi wa Mtibwa umesema kwa sasa wataanza kufanya mazungumzo na Santos kuwalipa fedha zao ambazo ni gharama za safari na malazi huku wakishirikiana na TFF.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupitia TFF walisema Mtibwa wanapaswa kuwalipa Santos kiasi hicho cha fedha ili kuweza kupata nafasi ya kucheza mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika yanayoanza Disemba mwaka huu.
Mtibwa walifungiwa kushiriki mashindano hayo baada ya kushindwa kukipelekea kikosi chao mwaka tajwa juu kwa ajili ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mchezo wa marudiano ikiwa ni baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 kwenye mechi ya awali jijini Dar es Salaam.
Ikumbukwe Mtibwa kwa Mujibu wa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, alitangaza kufikia Julai 20 wanapaswa kukamilisha malipo hayo, lakini baadaye wakaja kuwaongezea wiki mbili nyingine.
Mtibwa Sugar ilipata nafasi ya kuikwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka bingwa wa kombe la FA dhidi ya Singida United kwa ushindi wa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
0 COMMENTS:
Post a Comment