NINJA AIFICHA JEZI YA CANNAVARO
Jezi ya Yanga yenye namba 23 ambayo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alimkabidhi Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aendelee kuitumia baada ya yeye kustaafu kucheza soka, jezi hiyo bado ipo kabatini.
Cannavaro ambaye ni meneja wa Yanga kwa sasa, hivi karibuni alitangaza kustaafu kucheza soka akiwa nahodha wa timu hiyo ambapo uongozi ulitaka kuistaafisha jezi yake, lakini yeye akakataa na kumkabidhi Ninja.
Ninja ambaye alisajiliwa na Yanga msimu uliopita, bado hajaanza kuitumia jezi hiyo na wikiendi iliyopita kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger alivaa jezi yake namba 6 aliyokabidhiwa wakati anatua Yanga.
Kwa mujibu wa Gazeti la Championi, Ninja amesema jezi hiyo anasubiri kuanza kuitumia kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ambao unaanza leo huku Yanga ikicheza kesho Alhamisi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
“Unajua jezi niliyoachiwa na Cannavaro siwezi kuitumia kwenye michuano ya kimataifa kwa sababu kule natambulika ninaitumia jezi namba 6, lakini msimu wa ligi ukianza rasmi ndiyo nitaanza kuitumia.
“Ni jambo zuri kuona nimekabidhiwa jezi hii na mkongwe ambaye anaamini nitaitendea haki, hivyo nitajipanga kuhakikisha simuangushi,” alisema Ninja ambaye Kocha Mwinyi Zahera ameanza kumtumia kama kiungo lakini pia beki wa kulia.
0 COMMENTS:
Post a Comment