SARRI AKARIBISHWA EPL KWA MAUMIVU MAN CITY IKIITWANGA CHELSEA NGAO YA JAMII
Straika Sergio Aguero amefanikiwa kufunga mabao mawili ambayo kwake ni ya 200 na 201 akiwa ndani ya kikosi cha Manchester City, ambapo yamekuwa na msaada wa kuwapa ushindi wa mchezo wa Ngao ya Jamii.
Man City imepata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chelsea ambayo ilishuka uwanjani ikiwa chini ya Kocha mpya, Maurizio Sarri, leo Agosti 5, 2018 Jumapili.
Mchezo huo ambao unazikutanisha timu mbili zilizotwaa ubingwa wa Premier League na ile iliyobeba Kombe la FA ulikuwa mzuri lakini ni Man City ndiyo ambao walionekana kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Wembley.
Kipute hicho ni mchezo wa kuashiria kuwa ufunguzi wa Ligi Kuu ya England ‘Premier League’ unatarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa wiki hii.
Aguero ambaye msimu uliopita alikuwa na wakati mgumu kutokana na kuwa chaguo la pili nyuma ya Jesus kikosini kwake, alikuwa mwiba katika mtanange wa jana na alitumia uzoefu wake vizuri kuivuruga safu ya ulinzi ya Chelsea.
Kiungo mshambuliaji wa Man City, Bernardo Silva alikuwa na siku nzuri kutokana na kuonyesha ubora wa hali ya juu na kuwa nguzo kubwa katika kumuwezesha Aguero kufunga katika dakika ya 13 na 58.
0 COMMENTS:
Post a Comment