Mabingwa wa Soka Tanzania, Simba wamemtangaza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa, kuwa ndiye atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha Simba Day.
Simba Day itakuwa Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati Simba ikiivaa Asante Kotoko ya Ghana kwenye Uwanja wa Taifa.
Waziri Mkuu Majaliwa ni mwanamichezo, kwa kuwa ni kocha kitaaluma na pia mchezaji wa kikosi cha bunge na Simba imemualika kama kiongozi wa wananchi wa Tanzania katika Serikali ya awamu ya tano.
Sherehe maalum za Simba ambazo hufanyika kila mwaka ambapo klabu hiyo hutumia fursa ya kutangaza kikosi chao cha msimu na kutambulisha jezi zao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema Waziri Majaliwa ndiye atakuwa mgeni rasmi huku akiwataka mashabiki wa Simba popote walipo kujitokeza kwa wingi siku hiyo.
“Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ndiye atakuwa mgeni rasmi katika Simba Day tutakapocheza dhidi ya Asante Kotoko, siku hiyo ni maalum kwani itakuwa na vitu vingi ikiwemo kutambulisha wachezaji wetu wapya, hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kuona tukio hilo,” alisema Manara.
Manara alisema viingilio siku hiyo vitakuwa ni Sh 5000 kwa viti vya mzunguko, VIP B Sh 15,000 na VIP A Sh 20,000 ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Tundaman, Msaga Sumu, Mwasiti, Bendi ya Twanga Pepeta na nyingine nyingi.
0 COMMENTS:
Post a Comment