September 4, 2018






Si vibaya kukumbushana kuwa hatimaye uongozi wa Klabu ya Simba, umetangaza tarehe rasmi ambayo timu hiyo itafanya uchaguzi wa kuwasaka viongozi wake wapya.

Kamati ambayo imepewa dhamana ya kuongoza uchaguzi huo imetangaza Novemba 3, mwaka huu kuwa siku rasmi ya kufanyika kwa uchaguzi huo ambao fomu zake zitaanza kuchukuliwa leo Jumatatu.

Kabla ya kutangazwa kwa tarehe hiyo ya uchaguzi, klabu hiyo ilipewa siku 75 na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha wanafanya uchaguzi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kamati hiyo ya uchaguzi Simba, Boniface Lihamwike amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika siku hiyo huku kama mambo yakienda sawa watamtangaza mshindi siku hiyohiyo.


“Tunatangaza kwamba uchaguzi utakuwa Novemba 3, mwaka huu huku mchakato mzima ukianza kesho (leo) kwa wagombea kuchukua fomu.

“Kwa kutumia kanuni za TFF na katiba ya Simba ibara ya 27, nafasi ambazo zitagombaniwa ni sita, moja kati ya hizo mjumbe mmoja  atachaguliwa kama mwenyekiti (wa bodi ya wakurugenzi) na lazima awe na elimu ya shahada ya kwanza kutoka katika vyuo vinavyotambulika.

“Na kwa wagombea ambao watataka kugombea wao watalipa laki tano kwa ajili ya kuchukua fomu lakini ukiondoa mwenyekiti kuna nafasi ya mjumbe mwingine ambaye naye atatakiwa awe na shahada ya kwanza ambayo inatambulika TCU.

“Pia kutakuwa na nafasi za wajumbe wanne ambao wenyewe wao sifa zao wanatakiwa wawe na elimu ya kuanzia kidato cha nne, ambao wenyewe wao fomu zao zitakuwa laki tatu. Kati ya wajumbe hao mmoja lazima awe mwanamke,” alisema Lihamwike.

Mchakato wa uchaguzi huo utaanza leo Jumatatu kwa wagombea kuchukua fomu hadi Septemba 10, kisha Septemba 11-15 kurudisha, Septemba 16-18 usaili wa wagombea na kubandika majina ya wanaogombea.

Septemba 21-23 pingamizi kwa wagombea, 24-26 kupitia mapingamizi, 27-29 kusikiliza na kutoa maamuzi, Oktoba 2 majina ya waliokidhi vigezo yatawekwa wazi kisha Oktoba 3 kufungua kampeni zoezi ambalo litadumu hadi Novemba 2, kisha Novemba 3 uchaguzi.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema: "Tunaomba Wanasimba ambao wana sifa za kugombea wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuijenga klabu yetu, kamati hii itakuwa huru na haitaingiliwa na mtu kwa jambo lolote lile, kikubwa tutakachokifanya ni kuwatimizia kile wanachokitaka.” 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic