KIONGOZI SIMBA AWEKEWA KIGINGI, AIBUNA NA LAKE
Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Simba, chini ya Mwenyekiti, Hassan Dalali, Mwina Kaduguda amewekewa pingamizi katika mchakato unaoendelea wa uchaguzi wa klabu hiyo lakini amefanikiwa kulipangua.
Kaduguda ni miongoni mwa wanachama 21 ambao walichukua fomu ya kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Klabu ya Simba katika nafasi ya ujumbe.
Pingamizi ambalo amewekewa Kaduguda linahusiana na madai ya kutowasilisha mahesabu ya mapato na matumizi kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo wakati wa uongozi wake.
Uchaguzi mkuu wa Simba unatarajia kufanyika Novemba 3, mwaka huu kuchagua viongozi wapya baada ya viongozi waliokuwa madarakani kumaliza muda wao ambapo uchaguzi huo utafanyika kwa kutumia katiba mpya ya klabu hiyo ya mwaka 2018 katika mfumo wa mabadiliko.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Boniface Lyamwike amesema, Kaduguda aliwekewa pingamizi linalohusu kutowasilisha mahesabu katika kipindi chake cha uongozi lakini amefanikiwa kupita.
“Kaduguda aliwekewa pingamizi kufuatia madai kwamba katika kipindi chake cha uongozi hakuweza kufikisha mahesabu ya mapato na matumizi katika mkutano mkuu wa Simba ikiwa ni kinyume na katiba ya klabu.
“Katika shauri hilo, Kaduguda amefanikiwa kushinda kufuatia mtu aliyemkatia pingamizi kutotimiza vigezo vya pingamizi kwa kutolipia ada ya pingamizi ambayo ni shilingi elfu hamsini kigezo ambacho alikitumia Kaduguda
katika kuwasilisha pingamizi lake kwa aliyemkatia pingamizi hivyo kusababisha ashinde.
“Kuna wagombea wengine wanne ambao shauri lao bado tunaendelea kulisikiliza ambapo tulianzia jana ‘juzi’ na leo ‘jana’ tunaendelea kusikiliza ambapo mapingamizi yao yanafanana na ya Kaduguda, hivyo tukikamilisha tutaweka wazi kwani tunahofia kuweka wazi sasa majina kwa kupoteza ushahidi,” alisema Lyamwike.
je hayo madai ni ya ukweli kama ni ya ukweli hamuoni mnampitisha mtu asiye na sifa kwenda kugombea
ReplyDelete