RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli jana ameikabidhi timu ya taifa, Taifa Stars Sh mil 50 ‘keshi’ kwa ajili ya kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye mbio za kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Afrika ‘Afcon’ huku akionya kuwa wakifungwa basi watazitapika.
Stars inayonolewa na Kocha Emmanuel Amunike raia wa Nigeria, bado ina nafasi ya kufuzu kucheza Afcon mwakani nchini Cameroon kwani ipo nafasi ya pili katika kundi lao ikiwa na pointi tano na sasa imebakiwa na mechi mbili.
Mechi hizo ni dhidi ya Lesotho ugenini na Uganda itakayopigwa hapa nchini.
wachezaji na benchi la ufundi la Stars walialikwa jana Ikulu kupata chakula cha mchana na Rais Magufuli lengo ni kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoianza na pia kuwataka wafanye vizuri pale palipobaki ili watinge kwenye fainali hizo.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Dk Augustine Mahiga ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga.
Akikabidhi fedha hizo kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia aliyekuwa na katibu wake, Wilfred Kidao na nahodha wa Stars, Erasto Nyoni, Rais Magufuli aliwataka kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya wachezaji na siyo watu binafsi, na kabla aliahidi atafuatilia kila senti.
Rais Magufuli alisema: “Fedha hizi milioni 50 nazitoa kwa ajili ya wachezaji kwenda kutafuta ushindi, mrudi na ushindi na kama mkishindwa mtazitapika kwa njia nyingine umesikia Mh Rais (Karia).
“Tunahitaji kuona timu hii inashinda na inarudi na ushindi, nitasikitika mkienda Lesotho mkafungwa na mkarudi na sababu zisizo za msingi, sitapenda kusikia hilo na mnatakiwa kujua Watanzania wanawategemea sana.
“Hili ndugu zangu ninawaambia sasa mmeingia kwenye mkataba wa ajabu, si mmekubali kuja hapa, nitafuatilia kweli, na hela hii mil 50 nitajua mpaka senti tano imeliwa wapi na ole wake waile, siwezi kutoa hela ya serikali,hela ya walipa kodi halafu wapeleke watu wengine wakachezee huko, nataka ikatumike kwenye matumizi ya hawa vijana.
“Kama ni kula,kula mpaka msuri unenepe kama kiazi ale hadi mguu uwe mkubwa akafunge magoli, Lesotho nao watufunge? Itakuwa ni aibu nitajuta kwa nini nilikuja kuwaona kwa sababu itatoka pale “Magufuli awapa mkosi vijana, wamepigwa 10,” tunatakiwa kubadilika.
“Hakuna kitu kinachoniumiza sana kama kushindwa. Huwa ninajisikia vibaya kwa sababu ninafahamu Tanzania tangu tupate uhuru tulikuwa mil 10 na leo tupo mil 55, ni aibu kwa watu mil 55 kushindwa kupata wachezaji 11 wanaoweza kuwaletea kombe hata la Afrika, hicho nasema kwa dhati huwa kinanisononesha.
“Nina uhakika kusononeka kwangu siyo tu kwangu tu, Watanzania wengi wamekata tamaa kushabikia hata timu za ndani, ndiyo maana wengi wanataja majina ya wachezaji wa nje, unaweza kukuta wanazungumzia juu ya wachezaji wa Arsenal, Manchester n.k.
“Nakuamini kocha Amunike, naamini utaibadilisha timu yetu na kuweza kufikia malengo, natamani kuiona Tanzania inaenda Cameroon na huko ikurudi na ushindi.”
Aidha Rais Magufuli aliwaomba Waziri Mwakyembe na Mahiga na Tenga kushughulikia fedha ambazo zilinyimwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa ‘Fifa’ kutokana na kuwa na matatizo ili ziweze kuanza kutolewa na kuongeza kuwa kama kuna baadhi ya watu bado wapo na kusababisha fedha hizo zisitolewe basi atakuwa tayari kuwapeleka mahakamani wote.
Kwa upande wake Nyoni ambaye alimkabidhi zawadi ya jezi Rais Magufuli, alimshukuru kiongozi huyo kwa kitendo cha kuwaalika Ikulu huku akiahidi kuwa watapambana kuhakikisha wanafanya vizuri.
Naye Kocha Amunike aliahidi ushindi na kusema kuwa wanataka kutengeneza historia ya kushiriki Afcon kwani mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1980.
0 COMMENTS:
Post a Comment