October 10, 2018







Na Saleh Ally
SINGIDA United ni moja ya timu kubwa hapa nchini na unaweza kuona mambo yameenda haraka sana, ni ndani ya kipindi cha muda mfupi sana.

Imekua kwa muda mfupi na Singida United inatambulika namna hiyo, nafikiri inatokana na namna ambavyo viongozi wake wamekuwa makini mara tu baada ya timu hiyo kurejea Ligi Kuu Bara.

Singida United si wageni katika ligi hiyo kwa kuwa wamekuwa ni wale wanaopanda na kuporomoka na kama kuna mtu anaifahamu ile  Singida United ya miaka ile, basi atakuwa anaelewa vizuri tofauti kubwa iliyopo sasa.

Nafikiri viongozi wa Singida United hata kama kuna sehemu watakuwa wanakosea kama wanadamu wanastahili pongezi kubwa kwa kile walichokifanya na kikubwa kwao, wajue wana deni kubwa zaidi la kuifanya klabu yao kubaki katika kiwango kilichopo sasa, halafu waendelee kuongeza.

Nimeanza kuitaja Singida United kwa kuwa nilikuwa nimelenga kumzungumzia mchezaji wao mpya, huyu ni kijana Geofrey Mwashiuya.

Mwashiuya aliamua kuondoka Yanga na kujiunga na Singida United. Huenda aliwashangaza wengi kwamba Yanga ni timu kubwa zaidi na alikuwa bado anahitajika.

Wakati anaondoka Kocha George Lwandamina, Mwashiuya tayari alianza kupoteza mvuto wa kutegemewa kama ilivyokuwa awali. Unakumbuka alivyotua Yanga akitokea timu ya Kimondo FC iliyomkuza?

Kama unakumbuka wakati akitua Yanga, alibatizwa jina la Lunyamila. Hii ilikuwa picha njema kwake, sasa mambo yamebadilika na sivyo ilivyotarajiwa.

Kocha Lwandamina, binafsi namuona mmoja wa makocha bora kabisa waliowahi kuinoa Yanga. Alikitambua kipaji cha Mwashiuya na alimpa nafasi kubwa sana ya kuonyesha alichonacho na hakika alifanya hivyo.

Mwishoni alianza kuonekana anapotea njia. Hata alipopata ukali wake, nafasi ya kufanya kilichoonekana ni kikubwa haikuwepo tena na niwe wazi, akawa ni mchezaji wa kawaida, au tumia neno asiyetisha tena.


Unapokuwa unacheza mbele, halafu hautishi, basi ujue kuna tatizo kubwa. Maana hata walinzi tu hasa wa kati wanatakiwa kutisha ili kupunguza makali ya washambuliaji wabishi au wasumbufu. Sasa vipi wewe unaisaidia timu yako kushambulia, halafu hautishi?

Mwashiuya hatishi tena, hata huko Singida United, hatishi. Si yule ambaye timu itakapokutana na Singida United itakuwa na hofu kwa kuwa wanaye Mwashiuya na hii ni kengele ya upepo mbaya kwake ambao kama ataendelea kuupa nafasi, utamchota.

Sina maana Mwashiuya si mchezaji mzuri, lakini leo nimetaka asome hapa ili ajipime. Singida United wamecheza mechi tisa, yeye amecheza sita na karibu zote amekuwa akishindwa kumaliza muda wote.

Naona mara nyingi kocha Hemed Morocco akimtoa Mwashiuya na kumuingiza kinda Tibar John ambaye ana kipaji kikubwa licha ya upungufu mwingi wa kiufundi kama kutokuwa makini au kucheza mpira wa kikubwa au kutokuwa na nguvu za kutosha, nikimaanisha anahitaji mazoezi zaidi kuwa imara zaidi.

Pamoja na hivyo, Tibar ni mchezaji bora kabisa na Mwashiuya anashindana na kijana mwenye uwezo mkubwa. Hakuna ujanja, lakini afanye kila linalowezekana kurudi na kuwa Mwashiuya anayeisaidia Singida United, tishio Tanzania Bara ili apate nafasi ya kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars.

Umri wa Mwashiuya, hapaswi kuwa anatolewa. Anatakiwa ategemewe kuwa atafanya lolote wakati wowote na kocha awe na hofu ya kumtoa kwamba kumuacha nje ni hasara.

Sina maana Tibar asicheze, mechi ziko nyingi sana. Lakini Mwashiuya anapaswa kuonyesha thamani yake sasa kabla mambo hayajaharibika kabisa.


Uwezo anao lakini anatakiwa afanye zaidi. Mwashiuya bado hajaonyesha alichonacho. Ubora wa kipaji chake unaweza kulindwa na mazoezi zaidi, hasa yale ya ziada lakini pia nidhamu ya juu.

Kipaji bila juhudi na nidhamu, kamwe huwa hakifiki mbali. Mwashiuya uwezo anao lakini kwa umri alionao, ana nafasi ya kujitazama upya tena.

Aina ya uchezaji wa Mwashiuya ni kasi na nguvu. Kuwa imara katika kiwango sahihi lazima ahakikishe anajituma zaidi na kuwa na mwili ulio sahihi kwa kazi anayoifanya.

Nimkumbushe tena, kwa hali inavyokwenda, Singida United inaonekana ni timu yenye nafasi nzuri zaidi kwa wachezaji kutoka, nikiwa na maana ya kufanikiwa. Hivyo aongeze juhudi zaidi na zaidi.



1 COMMENTS:

  1. Saleh kwenye maisha ya mpira mchezaji anatakiwa kuwa na nidhamu ya ndani na nje ya uwanja. Maisha ya mchezaji na kitu gani anafanya akiwa mtaani yana impact kubwa ndani ya uwanja. Huyu bwana ana laana ya mzazi mwenziwe, nilitazama story hii hapa : https://www.youtube.com/watch?v=NbkTODzUlDs ikanishangaza. Kwa sisi tunaoamini Mungu tunakusahuri ongeza paragraph kwenye article yako kumshauri huyu bwana atubu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic