October 5, 2018






NA SALEH ALLY
NILIREJEA kuangalia mechi ya watani wa jadi kati ya Simba dhidi ya Yanga ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana.


Ilikuwa ni mechi nzuri kwa maana ya burudani ya mchezo wa soka kwa kuwa kila upande ulitaka kufanya vizuri.


Ilionekana Simba walikuwa wana nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo kwa kuwa kikosi chao kilicheza kwa kiwango kizuri zaidi ya wapinzani wao Yanga.
Ukiangalia vizuri, kilichowaangusha Simba ni aina ya uchezaji, hawakuwa makini hasa katika suala la umaliziaji walipokuwa wakisukuma mashambulizi yao kwenda kwa Yanga.


Maana katika utengenezaji nafasi, wao walifanya vizuri zaidi, lakini wakakumbwa na ugumu wa umaliziaji. Hata kama kipa Beno Kakolanya alikuwa katika kiwango kizuri, lakini bado suala la kumalizia au umakini katika umaliziaji, haukuwa mzuri hata kidogo.


Ukiachana na mchezo kwa jumla, nimeamua niingie katika ule mjadala ambao umejitokeza. Hapa ni kuhusiana na mchezaji wa Simba, beki na kiungo kiraka James Kotei.


Kotei alionekana akimtwanga beki wa Yanga, Gadiel Michael, sijui niseme kofi au ngumi, lakini kwa kifupi amempiga wazi kabisa na si suala la kujiuliza mara mbili kama lilitokea au la.


Kotei, raia wa Ghana, alikuwa akiwania mpira na Gadiel. Waligongana lakini baada ya hapo aligeuka na kumpiga mwenzake katika kiwango ambacho katika mchezo wa soka hauwezi kusema ni sahihi au bahati mbaya.


Alichokifanya Kotei, inaonekana wazi alikusudia kwa kuwa tu alishikwa na hasira na kushindwa kujidhibiti. Hakuna ubishi, kweli alikuwa na hasira lakini hicho hakiwezi kuwa kigezo cha kusema anapaswa kuachiwa.

Nimeona mijadala mingi kuhusiana na hilo, tayari mashabiki wanaona si sawa afungiwe na wengine wa Simba wamekuwa wakisambaza video beki wa Simba, Mohammed Zimbwe ‘Tshabalala’ wakiangushana na Vicent Andrew ‘Dante’ na baadaye Dante alitaka kumpiga kichwa lakini akamkosa.


Yote hii ni kuonyesha kwamba pia kuna mchezaji wa Yanga alikosea. Ishu hii sasa imegeuka kama vile ushindani wa kuonyeshana makosa.

Pia inawezekana kwa yule atakayeonyesha ukweli au kusisitiza hatua ichukuliwe ataonekana mbaya. Kwa hali yoyote, bila ya kupepesa au chembe ya woga ni hivi; Kotei anapaswa kuadhibiwa.


Binafsi namfahamu Kotei kama mmoja wa wachezaji wenye nidhamu sana. Ndani na nje ya uwanja, si mtu anayependa makuu, si mkorofi na mpambanaji.

Unaweza kusema kama mwanadamu alizidiwa hasira lakini yote haya, hayazuii au kubadilisha kwamba alifanya kosa na anastahili adhabu ili kudumisha adhabu na kutengeneza usawa kwa wengine.

Nililivalia njuga suala la Juma Nyosso kumdhalilisha John Bocco. Nilieleza namna tunavyopaswa kuwa na nidhamu ya juu katika klabu, ndani ya timu na kwenye ligi yetu.

Unakumbuka, hata baada ya Asante Kwasi, beki Mghana wa Simba kutemewa mate na Kelvin Yondani wa Yanga nilisisitiza suala hili tena kwa msisitizo wa juu.


Nilipata maoni ya watu kadhaa wasiojitambua kwamba nashinikiza Yondani afungiwe. Binafsi bila ya woga, nasisitiza nilitaka aadhibiwe kwa mujibu wa kanuni na si kufungiwa. Kama unakumbuka Yondani alisimamishwa mechi tatu.


Leo, bila ya woga hata kidogo, msisitizo wangu ni huohuo kwamba Kotei amefanya jambo la kipuuzi ndani ya  mchezo wa soka. Hata kama amekuwa mtu mwema kabla, lakini shambulizi lile kwa Gadiel, basi anastahili adhabu.

Mpira hauwezi kukubali watu wapigane ngumi. Nimeshangazwa na mwamuzi Jonesia Rukya, alionekana wazi aliliona kosa hilo.

Hivyo TFF na Bodi ya Ligi, wanapaswa kuchukua hatua ili kuwaonyesha wengine kuwa suala la nidhamu linapewa kipaumbele na wale ambao wanatetea, basi wajifunze kuweka ushabiki kando na waangalie suala la nidhamu kama chachu ya kuwapa mafanikio.


9 COMMENTS:

  1. UKO SAHIHI SANA UKWELI UNAUMA LAKINI LAZIMA TUUSEME KOTEI KAFANYA JAMBO LISILO LA KIUNGWANA TFF WACHUKUE HATUA STAHIKI KUKOMESHA TABIA HIZI BILA UPENDELEO WOWOTE.

    ReplyDelete
  2. Lakini mimi bado najiuliza kwanini kile kitendo cha Ngoma kumpiga khassan Kessy kilipita hivihi na kusahaulika bila kuchukuliwa hatua yoyote? Angalau hata Kotei kaonesha uungwana wa kumuomba radhi mchezaji mwenzake na watu wa kumuadhibu au kutokumuadhibu kotei ni TTF au bodi ya ligi na nnaimani wapo kwenye mchakato wa suala hili sasa nyinyi mnaotokwa na mapovu kushinikiza kuwafundisha kufanya kazi yao sijui mnakusudia kitu gani?

    ReplyDelete
  3. Acheni ushabiki...Yondani mtema mate alipata adhabu gani...baada ya mechi alikuwa na kadi mbili...halafu akaigomea tanga sababu ya malipo...hakupata adhabu yeyote

    ReplyDelete
  4. Dante kotei wote wataadhibiwaa mbona mwenyekit Alisha sema

    ReplyDelete
  5. Wote waliofanya makosa wanapaswa kuadhibiwa na siyo Kotei pekee yake hata Dante pia apewe adhabu.

    ReplyDelete
  6. Nilitegemea kuona mwandishi akigusia na kichwa cha kihuni cha Dante. Tuache ushabiki, tuache kutajataja majina kinazi, kama umeamua kusema ukweli sema ukweli wote

    ReplyDelete
  7. Kama waandishi tutafanyakazi ya sheria (hakimu), uongozi wa TFF na hata ukocha itakuwa ngumu sana kuwa na weledi unaostahili.

    ReplyDelete
  8. Kama ni suala la kuadhibiwa ataadhibiwa na wenye mamlaka na wala si kushinikiza mamlaka zifanya mtakacho. Mbona hamsemi Dante aadhibiwe? Pumba tu mnatafuta ulaji kwa matukio. Simple mind discusses people, average mind discusses events

    ReplyDelete
  9. Soka labongo linaukakasi Sana hayo mambo huwa yanajitokeza marakwa Mara lakin Hakuna azabu Kari inayo toka hivyo itaendela tabia hiz nizakuzifyeleeea mbali

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic