October 5, 2018


Nyie si mnasema kuwa kiungo Mkongoman, Papy Kabamba Tshishimbi anajua? Sasa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amewaambia viongozi kwamba anashusha bonge la kiungo fundi zaidi yake.

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo ilazimishe suluhu dhidi ya watani wao wa jadi, Simba walipokutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo, kocha huyo alisikika akiisifia safu ya kiungo ya Simba iliyokuwa inachezwa na Jonas Mkude na Mzambia, Claytous Chama kuimiliki sehemu hiyo ya kiungo huku akiwa hafurahishwi na anachofanya Tshishimbi.

Habari za uhakika ambazo Spoti Xtra imezipata ni kwamba Kocha huyo anayeongea lafudhi ya Kikongo baada ya mchezo na Simba aliwaambia viongozi wa timu hiyo kuwa ni lazima wapate kiungo mwingine mkabaji mwenye uwezo mkubwa zaidi ya Tshishimbi na wakubwa hao wamemkubalia ingawa bado wanajiuliza mtu mashine zaidi ya Papy si itakuwa balaa?

Habari zinasema kwamba kiungo huyo ambaye tayari Zahera anaye atamwaga wino Yanga wakati wa dirisha dogo linalofunguliwa Novemba 15.

“Kocha amekuwa akichukizwa na aina ya uchezaji wa Tshishimbi wa kufanya majukumu ambayo siyo yake katika mechi, hivyo anamtaka kiungo fundi atakayefanya kazi yake vizuri bila ya kumchosha Fei Toto,”alidokeza kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Yanga.

“Kocha huyo ametuambia kuhusiana ujio wa kiungo huyo na kilichobakia ni viongozi tu kupitisha usajili huo na huenda wakati huo hata Mwenyekiti Yusuf Manji atakuwa amesharudi klabuni,”aliongeza.

ZAHERA ANASEMAJE?

“Hizo taarifa umezitoa wapi? Ni kweli kabisa wewe mwenyewe ni shahidi timu umeiona bado haipo vizuri, hivyo ninahitaji kukifanyia marekebisho kikosi changu katika usajili wa dirisha dogo.

“Moja ya sehemu ambayo inayohitaji kufanyiwa marekebisho ni safu ya kiungo, kama unavyomuona Tshishimbi anashindwa kutimiza majukumu yake vizuri vile inavyotakiwa.

“Ulishawahi kumuona Kante (N’golo) akicheza uwanjani? Ndiyo ninataka kiungo mkabaji wa aina hiyo ambaye yeye kupiga chenga kwake hadi itokee, lakini siyo kama Tshishimbi ambaye yeye anajisahau na kujifanya Messi (Lionel) anapiga chenga hadi anapitiliza,”alisema Zahera ambaye amekwenda kwao DR Congo kuiandaa timu ya Taifa itakayocheza na Zimbabwe nyumbani na ugenini.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya amesema kuwa; “Zahera amedhihirisha kwamba yeye ni kocha bora na ameweza kutimiza baadhi ya malengo ya timu kutokana na pale ilipokuwa nyuma na ilivyo hivi sasa ameonyesha mabadiliko makubwa sana kutokana na kukiimarisha kikosi.”

“Hivi ndivyo tulivyokuwa tukihitaji kikosi chetu kiwe, kwani hakuna aliyetegemea matokeo tunayoyapata mashabiki walikuwa wakihofia kuchangia kutokana na kuona kwamba hatuna kikosi kizuri.

“Mwalimu ni bora na amedhihirisha ubora wake kutokana na matokeo tunayoyapata, tukiimalisha vitu vidogovidogo kikosi chetu kitakuwa bora zaidi, tutahakikisha tunatoa ushirikiano kwa kumpatia vitu ambavyo anavihitaji tutaendelea kuwa bora zaidi ikiwemo kambi bora,” alisema Kaya.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic